1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wademokrat wamuidhinisha rasmi Hillary

27 Julai 2016

Bi Hillary Clinton ameidhinishwa rasmi na wajumbe wa chama cha Democratic nchini Marekani na kuwa mwanamke wa kwanza katika historia ya nchi hiyo kuwania nafasi ya urais kwa tiketi ya chama kikubwa cha kisiasa

USA Wahlen Hillary Clinton Präsidentschaftskandidatin Archiv
Picha: Reuters/L. Jackson

Bi Hillary Clinton mwenye umri wa miaka 68 na mke wa Rais wazamani wa Marekani Bill Clinton alishinda kinyanganyiro hicho baada ya kukabiliana na upinzani mkali katika hatua ya mchujo kutoka kwa aliyekuwa mpinzani wake Seneta Bernie Sanders.

Baada ya wa wafuasi wa Hillary Clinton na Bernie Sanders kutoleana maneno ya kejeli shangwe ziliripuka katika ukumbi wa mkutano mkuu huo mjini Philadelphia baada ya Hillary Clinton kutangazwa kushinda idadi ya kura 2,382 za wajumbe zilizohitajika ili kumuwezesha kuidhinishwa kuwania nafasi hiyo ya urais katika uchaguzi utakaofanyika mwezi Novemba mwaka huu.

Kwa hatua hiyo Hillary Clinton sasa atachuana na mgombea wa chama cha Republican Donald Trump ambaye pia alipitishwa na chama chake wiki iliyopita kupeperusha bendera ya chama cha Republican katika uchaguzi huo wa mwaka huu.

Picha: Reuters/J. Young

Akizungumza mbele ya wajumbe wa mkutano huo mkuu wa chama cha Democratic, Rais wazamani wa Marekani Bill Clinton alimwagia sifa mkewe na kusema ni mwanamke mwenye huruma na mtu mwenye uwezo wa kuleta mabadiliko ambaye taifa la Marekani linamuhitaji kwa sasa.

" Hillary Clinton ni mwanamke ambaye anapendelea siku zote kusogeza mpira mbele, hivyo ndivyo alivyo" alisikika Bill Clinton na kuwafanya wajumbe wa mkuano huo kuvutiwa na hotuba yake aliyoitoa kwa muda wa dakika 45. Aliongeza kuwa Hillary Clinton kwa sasa anasifa ya kipekee ya kushika nafasi hiyo nzito kwani bado anasifa hiyo ya kuleta mabadiliko na kuepusha hatari ambazo Marekani ingeweza kukabiliana nazo. Aidha Bill Clinton alikumbushia enzi za kipindi cha uchumba wao na Hillary miaka zaidi ya 40 iliyopita na kusema kuwa alivutiwa na sifa yake ya kuwa mwanamke ambaye anapendendelea kufanya mazuri kwa taifa lake.

Kwa upande mwingine Bill Clinton alionekana kumtupia vijembe ingawa pasipo kumtaja jina mgombea wa chama cha Republican Donald Trump pale alipoziponda sera zake zenye utata ikiwa ni pamoja na matamshi yake ya kuwapiga marufuku waumini wa dini ya kiisilmu kuingia nchini humo endapo atachaguliwa.

Baadhi ya wafuasi wa seneta wa jimbo la Vermont Berinie Sanders walionekana kukosa furaha na kuonekana kuwa na nyuso za hasira kufuatia kushindwa kwa seneta huyo lakini hata hivyo hasira zao hizo zilionekana kuzimwa na shangwe za wafuasi wa Hillary Clinton katika ukumbi huo wa mktano.

Picha: Getty Images/AFP/N. Kamm

Baadaye Seneta Bernie Sanders alipanda jukwaani kwa lengo la kujaribu kuwaunganisha wajumbe wote wa chama hicho ambapo alipokewa kwa kelele nzito za shangwe pale alipotamka kumuunga mkono Hillary Clinton na kusema anapaswa kuteuliwa kuwania nafasi hiyo ya urais kwa tiketi ya chama cha Democratic.

Hillary Clinton ambaye hakuwepo kwenye ukumbi huo wa mkutano alijitokeza kwa wajumbe hao kwa njia ya video akiwa amependeza mara baada ya hotuba ya mumewe na kuwashukuru wajumbe hao kwa heshima kubwa waliyompa

Hata hivyo chama hicho cha Democratic kilikumbwa na msukosuko katika hatua ya mwisho ya kuelekea kuidhinisha jina la mgombea wa chama hicho baada ya kufichuliwa na kuchapishwa katika mtandao wa Wikileaks barua pepe ambazo zilionyesha chama hicho kumpendelea zaidi Hillary Clinton wakati wakati wa kipindi cha kampeni hali iliyopelekea kujiuzulu kwa mwenyekiti wa kamati ya kitaifa ya chama cha Democratic.

Mwandishi: Isaac Gamba/ AFPE
Mhariri:Josephat Charo