Rais Yoon wa Korea Kusini atakiwa ajitokeze kuhojiwa
17 Desemba 2024Mahojiano hayo ni kuhusiana na tangazo lake lililoshindwa la kuanzisha utawala wa amri za kijeshi. Hayo yameripotiwa na shirika la habari la Korea Kusini, Yonhap, leo Jumanne.
Yoon, ambaye anasubiri uamuzi wa Mahakama ya Katiba kujua hatma yake, anachunguzwa kwa makosa ya kufanya uasi dhidi ya dola kutokana na kutangaza kwake sheria ya kijeshi mapema mwezi huu.
Yeye pamoja na maafisa wengine kadhaa huenda watakabiliwa na kifungo cha maisha jela au hata adhabu ya kifo iwapo watapatikana na hatia. Hii leo waendesha mashtaka wametaka Yoon kufika mbele yao kwa mahojiano kabla ya mwishoni mwa juma, ombi ambalo limekataliwa na ofisi ya mwanasiasa huyo. Wamesema iwapo atashindwa kufanya hivyo anaweza kukamatwa.
Hapo jana Mahakama ya Katiba ya Korea Kusini ilianza kusikiliza shauri la kuondolewa madarakani kwa Yoon na itakuwa na muda wa hadi miezi sita kuamua iwapo ataondolewa kikamilifu madarakani au atejea ofisini.