1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UtamaduniAfrika

Waendeshaji utalii Afrika wanahitaji wageni wa ndani

6 Mei 2022

Huku utalii wa kimataifa ukiwa bado umedorora, kampuni za utalii za Kiafrika zinahitaji wageni wa ndani ili kuchochea utalii. Lakini wengi katika bara hilo hawana uwezo wa kusafiri.

Tourismus in Afrika | Viktoriafälle, Uganda
Watalii wakiwa maporomoko ya Victoria kasakazini-magharibi mwa Uganda.Picha: Yasuyoshi Chiba/AFP/Getty Images

Mto Zambezi unatanda mandhari nzuri ya mpaka baina ya Zambia na Zimbabwe. Kisha, karibu na mahala paitwapo Livingstone, kituo cha utalii kwa eneo masikini la Zambia, na kwenye kilele cha mlima wa nchi jirani ya Zimbabwe, maji yanayovuma kwa kasi ya mto huo humiminika kwa umbali wa mita 110. Hapa yanaunda kile kiitwacho Maporomoko ya Victoria, maporomoko makubwa kabisa ya maji barani Afrika.

Wazimbabwe na Wazambia wengi hawawezi kumudu ada za kuingilia katika bustani kuona maporomoko ya maji ya Victoria, na fursa nyingi za kuyaona maporomoko ya mto yapo mikononi mwa makampuni binafsi, kama vile mabaa na nyumba za kulala wageni za watalii.

Uingiaji bado ni ndoto kwa wenyeji

Gift Kashimbaya anaishi katika mji wa Livingston nchini Zambia, dakika chache kutoka kwenye maporomoko hayo. Anaeleza kwamba ni lazima mtu apitie baadhi ya nyumba za kulala wageni ili kuona sehemu bora zaidi ya mto Zambezi kutokea Livingstone. "Na wakati mwingine unaweza kwenda mpaka wa Zimbabwe ambapo unaweza kulipa ada fulani," aliongeza.

Soma pia: Maonyesho ya utalii ya nchi za Afrika Mashariki mjini Arusha

Mfanyabiashara wa utalii wa Zambia Donald Chomba anasema ni tatizo kwamba wenyeji mara nyingi wanafungiwa nje ya maeneo ya umma na wafanyabiashara binafsi na waendeshaji watalii.

Maporomoko ya Victoria, ambayo ndiyo makubwa zaidi duniani yanakatiza kati ya Zimbabwe na ZambiaPicha: picture-alliance / dpa

"Hiyo ndiyo sababu kwa nini utalii wetu wa ndani hautaingia sokoni kamwe. Sitashangaa kama robo tatu ya wakazi wa Zambia hawajui ni nini kilichoko Maporomoko ya Victoria," Chomba aliiambia DW.

"Kwa nyumba za kulala wageni kuanze kuwazuwia wenyeji kuingia au kuwafanya walipe ili tu kuingia kwenye eneo hilo, nadhani hilo ni kosa."

Watalii wa kigeni ndiyo wanaopendelewa

Katika mji mkuu wa Zambia Lusaka, mfanyabiashara Brian Sakala anaishutumu serikali kwa kuegemea upande mmoja katika jinsi inavyokuza utalii na kupendelea wageni.

"Si busara kwako kutoa motisha kwa wageni na unawaacha watu wako," Sakala alisema. "Mungu ametubariki kwa vitu hivi vyote ili sisi sote tufurahie."

Kusaidia soko la ndani katika nchi za Afrika sasa ni muhimu zaidi kuliko hapo awali, kulingana na Hermione Nevill, mtaalam wa utalii wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC), shirika mbia la Benki ya Dunia.

"Hapo awali, iliwekezwa kidogo sana katika utalii wa ndani na wa kikanda barani Afrika kwa ajili ya watalii wa kimataifa wenye gharama kubwa," Nevill aliiambia DW.

Watalaii wanaokwenda Ghana wanaweza kufurahia fukwe zake na vituo vya turathi.Picha: atosan/IMAGO

Janga la COVID-19, pamoja na vizuizi vyake vya kusafiri, lilionyesha ni kiasi gani nchi za Kiafrika zilitegemea watalii wa kigeni.

"Wakati janga hilo lilipotokea, maeneo mengi yaligundua kuwa yanahitaji watu wa eneo hilo kusafiri lakini hawakuwa na data au taarifa kuhusu masoko haya," Nevill alisema. "Hii inafanya maeneo ya Kiafrika yasiwe na ustahimilivu kuliko washindani wenye tamaduni za kusafiri za ndani."

Kuweka vivutio kwa wageni wa ndani

Kulingana na Shirika la Fedha la Kimataifa, utalii umekuwa muhimu kwa uchumi wa Afrika katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.

Mnamo mwaka wa 2019, sekta hiyo ilichangia takriban asilimia 7 ya pato la jumla la Afrika na ilichangia dola bilioni 169 (€ 160 bilioni) katika uchumi wa bara hilo. Hiyo ni sawa na Pato jumla la ndani la mataifa ya Ivory Coast na Kenya.

Mnamo 2019, wasafiri wa kimataifa milioni 10 walitembelea Afrika. Hii ilishuka sana hadi milioni 2.3 mnamo 2021 kwa sababu ya janga hili.

Mwaka huu, hata hivyo, idadi ya watalii wa kimataifa kote barani Afrika inaongezeka, alisema Hanneli Slabber, mkuu wa masoko katika idara ya utalii ya Afrika Kusini.

Kwa upande wake, Afrika Kusini inaangazia soko la ndani ili kufufua sekta hiyo kiendelevu, mpango ambao nchi hiyo ilipitisha mwaka wa 2020.

Nigeria ina viwanja tisa vya kimataifa vya ndege na vinwaja vingine vingi vya ndani.Picha: Benson Ibeabuchi/AFP/Getty Images

"Janga hili lilisababisha Waafrika Kusini zaidi na zaidi kupata safari za siku, baadhi yao ni watu wa mara ya kwanza, watu ambao hawajawahi kufikiria safari kwa madhumuni ya burudani," Slabber alisema. "Tumejitahidi kuhakikisha kwamba watu wanajua kuhusu uzoefu tofauti, ikiwa ni pamoja na ule ambao ni wa bure kabisa."

Mnamo Februari 2022, wenyeji milioni 1.1 walisafiri ndani ya Afrika Kusini ikilinganishwa na 750,000 mwaka uliopita, Slabber anasema.

'Khaki safari' inatoa njia kwa 'Afrofuturist'

Mtaalamu wa utalii Nevill anasisitiza kuwa kukua kwa safari za ndani barani Afrika ni jambo gumu sana.

Barani Afrika, utamaduni wa usafiri wa ndani ni mdogo sana kwa kuanzia, Nevill alisema, na hii inafanya sekta ya utalii wa ndani kuwa hatarini zaidi kwa mambo kama vile uchumi dhaifu au kupanda kwa gharama za maisha.

Soma pia: Ukame waathiri utalii Afrika Kusini

Afrika Kusini ilikuwa mojawapo ya nchi za kwanza katika kanda hiyo kuwa na mkakati wa kitaifa wa utalii wa ndani.

Mfano mmoja wa mkakati huu ni kampeni ya usafiri ya "Sho't left," ikimaanisha "karibu sana" katika lugha ya kienyeji, ambayo inahimiza wenyeji kuwa watalii ndani ya Afrika Kusini.

Wakati wa wiki yake ya mauzo ya kila mwaka, ofisi ya utalii inatoa mikataba na vifurushi vya usafiri wa ndani, ambapo bei hupunguzwa hadi asilimia 50.

Wakati wa matukio mengine kama vile Mwezi wa Urathi wa Afrika Kusini, wenyeji wanapewa nafasi ya kuingia bila malipo kwenye makumbusho na bustani nyingi.

Milima ya Table inatazamana na mji wa Cape Town wa Afrika Kusini.Picha: Tibor Bognár/IMAGO

Nevill anasema uwekezaji unazidi kufanywa katika hoteli mpya zinazotoa uzoefu wa utalii wa asili ambao ni tofauti na safari za kitamaduni, ambapo watalii wa kimagharibi waliotoka katika mavazi ya safari ya nyakati za ukoloni wanaendeshwa kupitia mbuga ya wanyama.

Soma pia: Matumaini ya kuimarika kwa utalii Afrika Mashariki

Soko jengine linaloibukia kwa tabaka jipya la wasafiri, kulingana na Nevill, ni lile la watalii wachanga na wenye ujuzi wa kidijitali "Afrofuturist", ambao tayari wamezoea kusafiri kimataifa.

Dhana za masoko ya ndani

Masoko ya utalii wa ndani ya mataifa mengi ya Afrika ni madogo kuliko ya Afrika Kusini, ukiachilia mbali Kenya na Nigeria.

Pamoja na hayo, wakati wa janga la covid-19, nchi nyingi barani Afrika zilijaribu kukuza usafiri wa ndani na wa kikanda kwa kutoa nauli zilizopunguzwa zinazolenga watalii wa ndani, Nevill alisema.

Rwanda, kwa mfano, inashauriana na IFC juu ya mkakati wa maendeleo ya soko la ndani na kikanda lakini tayari inatoa bei tofauti kwa wageni wa ndani na wa nje.

Na huko Zambia, DW iliuliza nyumba za kulala wageni mbalimbali zinazomilikiwa na watu binafsi kwa nini wenyeji walihitaji kulipia kuingia, lakini haijapata jibu hadi wakati wa kuchapishwa kwa makala hii.

Mgahawa juu ya jiwe la baharini Zanzibar

02:45

This browser does not support the video element.

Wafanyakazi wa mamlaka ya utalii ya kitaifa walieleza wazi katika mazungumzo kadhaa ambayo hayajarekodiwa kuwa suala hilo lilikuwa muhimu, lakini DW haikuweza kupata taarifa rasmi ikiwa mamlaka ina mipango yoyote ya kuboresha hali hiyo.

Makala hii imeandaliwa na Glory Mushinge na Martina Schwikowski

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW