1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiEthiopia

Wafadhili waahidi dola milioni 630 kuwasaidia Waethiopia

17 Aprili 2024

Kongamano linaloungwa mkono na Umoja wa Mataifa limeahidi karibu dola milioni 630 za kuushughulikia mzozo wa kiutu nchini Ethiopia. Jumla ya nchi 21 zilitoa ahadi mpya zikiongozwa na Marekani iliyoahidi dola milioni 253.

Hali ya kibinaadamu Ethiopia
Kwa mujibu wa OCHA, "matukio ya kiangazi na mafuriko, na mapigano" yalichangia kuongeza hali kuwa mbaya EthiopiaPicha: Ed Ram/Getty Images

Kiasi hicho hata hivyo hakijafikia dola bilioni moja zinazotafutwakuwalisha mamilioni ya watu wanaokabiliwa na mizozo na mabadiliko ya tabianchi katika nchi hiyo ya pili yenye idadi kubwa ya watu barani Afrika.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Masuala ya Kibinaadamu Joyce Msuya amesema katika taarifa kuwa mchango huo ni mwanzo tu, na wanatumai kuendelea kuonesha uungaji mkono kwa mwaka mzima.

Soma pia: Je, mzozo wa njaa unaweza kuepukika nchini Ethiopia?

Mkutano huo wa wafadhili ulioandaliwa katika makao kuu ya Umoja wa Mataifa barani Ulaya jijini Geneva unataka kuchangisha fedha ambazo taasisi hiyo ya kimataifa inasema zinahitajika haraka ili kushughulikia msaada kwa miezi mitatu ijayo.

Madhila ya njaa Tigray baada ya vita

01:30

This browser does not support the video element.

Ethiopia yafunikwa na mizozo mingine.

Jumla ya nchi 21 zilitoa ahadi mpya, huku Marekani ambayo ni mfadhili mkuu wa Ethiopia, ikisema imeahidi dola milioni 253. Uingereza ambayo ilikuwa mwenyeji mwenza wa mkutano wa jana, iliahidi dola milioni 125, huku Umoja wa Ulaya ukisema kwa pamoja na nchi wanachama utatoa zaidi ya dola milioni 139.

Waethiopia wanakabiliwa na migogoro ya ndani wakati kukiwa na athari za kiuchumi na mabadiliko ya tabia nchi na mzozo unaozidi kuwa mbaya wa chakula na utapiamlo. Uingereza imesema Ethiopia inakabiliwa na hatari ya "kufunikwa na migogoro mingine ya kibinaadamu duniani kote.”

Marekani pia imesema kuwa inatoa dola milioni 154 za msaada wa kiutu ili kuyashughulikia mahitaji ya dharura yatokanayo na mzozo, ukosefu wa usalama na athari za mabadiliko ya tabia nchi. Wafadhili pia wameitaka serikali ya Ethiopia kuhakikisha utoaji wa misaada bila kuingiliwa. Mwaka jana Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani lilisimamisha misaada yote ya chakula kwa Ethiopia kwa miezi kadhaa baada ya uchunguzi wa ndani kubaini kuwepo kwa uporaji mkubwa.

(AP, AFP, Reuters, dpa)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW