Wafadhili wachangia dola bilioni 1.5 kuisaidia Sudan
20 Juni 2023Fedha hizo zitatumika pia kuyapiga jeki mataifa jirani na Sudan yanayowahifadhi mamia kwa maelfu ya watu waliokimbia mapigano.
Tangazo la mchango huo lilitolewa na mkuu wa misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths mwishoni mwa kongamano la siku moja lililofanyika mjini Geneva hadi jioni ya jana jumatatu.
Mkutano huo ulifanyika katikati ya utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano kwa muda wa siku tatu yaliyoafikiwa na pande hasimu nchini Sudan Jumamosi iliyopita.
Akizungumza mwishoni mwa mkutano huo Griffiths aliwakumbusha wafadhili kwamba licha ya michango iliyotangazwa, mzozo wa Sudan bado utaendelea kuhitaji fedha kwa kipindi cha muda mrefu.
"Tunatambua mshikamano tunaouona hii leo ni muhimu na ni ujumbe wa kuonesha ubinadamu na ukarimu. Ninayo heshima kutangaza kwamba wafadhili wamtakangaza karibu dola bilioni 1.5 za kusaidia shughuli za kiutu nchini Sudan . Mzozo huu utahitaji msaada endelevu wa kifedha na ni matumaini yangu sote tutaiweka Sudan juu kabisa ya vipaumbele vyetu" alisema Griffiths
UNHCR yahimiza fedha kutolewa haraka licha ya upungufu wa kinachohitajika
Kwa upande mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR, Filippo Grandi amewarai wote waliotoa ahadi za michango kuiwasilisha haraka iwezekanavyo kwa sababu tayari shughuli za kiutu nchini Sudan zinakabiliwa na ukata wa fedha.
Kulingana na Umoja wa Mataifa Marekani ndiyo imetangaza mchango mkubwa zaidi wa dola milioni 550 ikifuatiwa na Ujerumani itakayochangia dola milioni 162 na dola nyingije 151 zitatolewa na Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya.
Ingawa maafisa wa Umoja wa Mataifa walitoa shukrani kwa nchi wafadhili kwa mchango walioahidi, ukweli ni kwamba kiasi kilichotangazwa hakifiki hata nusu ya kile watoa misaada ya kibinadamu wamesema kinahitajika kwenye mzozo wa Sudan.
Tathmini ya hapo kabla inaonesha ni dola bilioni 2.6 ndiyo zinatakiwa kwa mwaka huu nchini humo kuwezesha kuwafikia wote wenye mahitaji.
Kuna kiwango kingine cha dola milioni 470 kilichopendekezwa mahsusi kwa mataifa jirani ya Sudan yaliyowapokea raia wa taifa hilo waliokimbia mapigano.
Miito ya kukomeshwa mapigano yatolewa huku hadi ikiwa tulivu Sudan
Kwenye mkutano huo kulikuwa pia na miito ya kuhakikisha mzozo wa Sudan unafikia mwisho.
Waziri Mkuu wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al-Thani alizirai pande zinazohasimiana kuweka mbele "maslahi ya raia wa Sudan" huku akizikumbusha kwamba hakuna suluhu ya kijeshi inayoweza kumaliza uhasama.
Kwa upande wake waziri wa mambo ya kigeni wa Misri Sameh Shoukry alizungumzia mashaka yaliyopo juu ya uwezekano wa mzozo unaoendelea kusambaa nje ya mipaka ya Sudan.
Shoukry alisema Misri inafuatilia kwa karibu kinachoendelea kwa sababu usalama na uthabiti wa Sudan ni muhimu kwa kanda hiyo.
Nchini Sudan kwenyewe hali ya utulivu imeendelea kushuhudiwatangu kuanza kutekelezwa makubaliano ya kusitisha mapigano hapo siku ya Jumapili.
Hakuna mashambulizi ya anga wala ya ardhini yaliyripotiwa na kwa jumla hali ilikuwa shwari kutwa nzima ya jana na usiku wa kuamkia leo.