Ujerumani: Waliopokea fedha za msaada watakiwa kuzirejesha
13 Oktoba 2025
Marion Alemeier mmiliki wa saluni moja Ujerumani bado anakumbuka Machi 23 mwaka 2020. Ilikuwa siku ya pili ya Ujerumani kutoa tangazo la watu kutokwenda kazini na kubakia majumbani ikiwa ni moja ya juhudi za kuudhibiti ugonjwa huo wa Covid 19. Waziri wa uchumi wakati huo Peter Altmaier anayetokea chama cha CDU na Waziri wa fedha wakati huo pia Olaf Scholz anayetokea chama cha SPD walitangaza ahadi kuwa kwa raia wa taifa hilo.
Katika msaada huo wa fedha kwa wafanyabiashara wadogo wadogo na watu waliojiajiri wenyewe Scholz alisema ni muhimu kwake kutoa msaada kwa watu hao na sio mkopo, kwahiyo inamaanisha pesa hizo hazistahili kulipwa. Katika tangazo hilo la Scholz waziri wa uchumi nae aliongeza sauti yake akiahidi kuwa serikali haitamuacha yoyote nyuma.
Zaidi ya miaka mitano baadae Marion Alemeier anahisi mzigo mkubwa umemlemea. Ameiambia DW kwamba ahadi nyingi zilitolewa lakini hakuna hata moja iliyofanikishwa. Ameongeza kuwa rafiki zake wengi na wafanyakazi wenzake walimuonya kuwa huenda akatakiwa kulipa fedha hizo ila hakuwaamini wakati huo alipopokea yuro 9000 kama msaada wa dharura, psa alizohitaji kutokana na watu kutakiwa nyumbani kwa wiki sita mfululizo na hakuwa na fedha za kutosha hadi Mei 4, 2020 ambako sheria kidogo zililegezwa na saluni Ujerumani zikaruhusiwa funguliwa tena.
Mahesabu hayakwenda sawa
Baadaye, ilitangazwa kuwa ruzuku hiyo ilikuwa imetolewa tu kulingana na makadirio ya kile kilichohitajika ili kuziba "pengo la ukwasi" lililosababishwa na janga hilo.
Sababu ya hii kutokea ni kwamba Wizara ya Uchumi ilikadiria kwamba kati ya euro bilioni 13 ambazo serikali za shirikisho na serikali za majimbo zililipa katika mfuko wa msaada wa dharura kwa miezi ya Machi hadi Juni 2020, kulikuwepo na euro bilioni 5 zilizoongezwa kimakosa na ndio maana barua za maombi ya kurejesha fedha zikatolewa kwa maelfu ya wafanyabiashara akiwemo Marion Alemeier, waliopokea kitita hicho kilichopaswa kuwa kiinua mgongo katika biashara zao.
Alemeier, alitakiwa kulipa yuro 7000. Mara moja alichukua hatua za kisheria na kushinda kesi hiyo lakini bado jimbo la North Rhine-Westphalian linataka kurejeshewa nusu ya pesa hizo yani yuro 3,500.
Watu waliojiajiri wenyewe kama Alemeier, walikuwa na uwezo wakati huo wa kuomba hadi 9000 za pesa hizo za dharura. biashara zilizowaajiri hadi wafanyakazi 10 zingeweza kuomba kiinua mgongo cha hadi yuro 15,000 na yuro 25,000 ziliweza kuombwa na wale waliokuwa na biashara zilizowaajiri zaidi ya watu 10 hadi 50. Kwa wengi hatua hii ya serikali ilikuwa msaada mkubwa lakini sasa hali imebadilika na wengi wamekasirishwa na hatua ya kutakiwa kulipa fedha ambazo awali waliahidiwa kuwa ni za msaada na sio mkopo.
Kila jimbo linatatua masuala yake tofauti
Kile kinachowakera wafanyabiashara hawa wadogowadogo na wale waliojiajiri wenyewe ni kwamba kila jimbo nchini Ujerumani lina uhuru wa kuamua mambo yake yenyewe na kwamba sheria sio sawa kati ya majimbo 16 yanayounda taifa la Ujerumani.
Kwa mfano katika majimbo ya Bavaria na Baden-Württemberg, wale walioangukiwa na shoka hilo la kulipa fedha hizo hawakuwa na nafasi ya kuukatia rufaa uamuzi huo na ilibidi wachukue hatua za kisheria haraka. Baadae mahakama ya Baden-Württemberg ilitoa hukumu yake dhidi ya kesi tano ambako wote hawakutakiwa kurejesha fedha hizo. Mahakama hiyo haikutoa sababu zake kutokana na kwamba bado keshi haijakamilika.
Katika jimbo la Hesse shauri hilo limesimamishwa kwa muda. Baadhi ya watu wanaona kana kwamba sasa wanasiasa wameshindwa kulishughulikia suala hilo huku baadhi wakisema mchakato wa kuomba fedha hizo ni mrefu na wa gharama kuliko fedha watajkapopata mwisho wa siku kama watafanikiwa.