1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafanyakazi wa kampuni ya madini wahojiwa Tanzania

21 Julai 2017

Serikali ya Tanzania imewataka wafanyakazi wa kigeni wa kampuni ya uchimbaji wa madini ya Acacia kuondoka. Mkurugenzi wa kampuni hiyo amekanusha taarifa na kusema anajadiliana na serikali.

Logo Acacia Mining

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo vyenye taarifa za kinachoendelea kwenye kampuni ya Acacia, wiki hii maafisa wawili waandamizi wa kampuni hiyo ambao ni wananchi wa Tanzania, walikamatwa na kuhojiwa katika uwanja wa ndege. 

Duru za karibu zinazoufahamu mzozo huo, zimeeleza kuwa kukamatwa kwa maafisa hao kunahusishwa na mzozo uliopo. Kampuni ya Acacia ndiyo mwekezaji mkubwa wa kigeni nchini Tanzania.

Akizungumza na shirika la habari la Reuters, Mkurugenzi mtendaji wa Acacia Mining Brad Gordon, amekanusha taarifa kwamba wafanyakazi raia wa Tanzania walikamatwa uwanja wa ndege. Hata hivyo amethibitisha kuwa waajiriwa wa kampuni yake wanaendelea kuhojiwa na vyombo vya usalama vya Tanzania. Aidha, Gordon pia amesema taarifa kwamba wafanyakazi wasio raia wa Tanzania wameamriwa kuondoka nchini si ya kweli. Hata hivyo, ameeleza kuwa kampuni yake imekuwa na wakati mgumu katika kujaribu kurefusha vibali vya wafanyakazi wa kigeni kuendelea kubakia Tanzania. 

Mikataba kusainiwa upya

Awali, kampuni hiyo ilikuwa imekubali kulipa kodi zaidi ili kumaliza mzozo na serikali inayodai kuwa kampuni hiyo imekuwa ikiripoti uzalishaji na faida ya kiwango cha chini kuliko ilivyokuwa kweli. 

Rais John Magufuli ameishutumu kampuni hiyo yenye makao yake makuu London kuiibia serikali na kukwepa kulipa kodi yenye thamani ya mabilioni ya dola za Kimarekani.

Tanzania hivi karibuni ilipitisha sheria mpya za kuratibu uchimbaji wa madini. Acacia imesema itaendelea kutathmini athari za sheria hiyo kwa kuzingatia makubaliano yaliyofikiwa awali kati ya kampuni na serikali. Magufuli anataka kila kampuni ya uchimbaji madini isaini mkataba mpya na serikali.

Tanzania ina utajiri wa madini na ni nchi ya nne kwa uzalishaji wa dhahabu barani Afrika. Kati ya madini ambayo Tanzania inauza nje, dhahabu ndiyo inazalishwa kwa kiwango kikubwa na ni chanzo cha msingi cha mapato. Tanzania pia inauza shaba, nikeli, almasi na tanzanite.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW