Mgomo tayari umeathiri sekta ya mafuta
26 Mei 2016Wafanyakazi katika vituo vya mitambo ya nguvu za Nyuklia nchini Ufaransa wanatarajiwa kujiunga na mgomo unaoendelea kuongezeka katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo ya kupinga mageuzi katika soko la ajira. Hadi kufikia alhamisi mgomo huo umeonekana kuleta athari katika usambazaji wa mafuta na uzalishaji wa umeme.
Zikiwa zimebaki wiki mbili kabla ya taifa hilo kuwa mwenyeji wa mashindano ya klabu bingwa barani Ulaya kwa mwaka 2016, nchi hiyo imejikuta katika mfululizo wa maandamano katika sekta ya usafiri na mafuta, ambao umeongeza shinikizo kwa serikali.
Vyama vya wafanyakazi vimeitisha maandamano mapya siku ya alhamisi katika miji kadhaa ya Ufaransa, machafuko hayo ya kijamii yaliyoanza miezi mitatu iliyopita yamegeuka sasa kuwa vurugu.
Waziri mkuu Manuel Valls hapo awali alisema kuwa sheria hizo za kazi zisingetolewa ila kuna uwezekano zingefanyiwa"mabadiliko"au"kuboreshwa."
Siku ya jumatano, Waziri mkuu huyo aliukemea Muungano wa wafanyakazi wa CGT ambao ndio unaoratibu maandamano hayo, akisisitiza kwamba wao "hawatungi sheria za nchi."
Katika maoni yake siku ya alhamisi , amesema muungano huo wa wafanyakazi "ulikosa uwajibikaji" na kusema tena kwamba hawawezi kulazimisha "kubadili sheria."
Kumeonekana kuwepo misururu mirefu ya watu katika vituo vya kuweka mafuta, wakati maeneo mengine yakianza kuwa na mgao wa mafuta baada ya pampu kuishiwa .
Wakati huo ambapo karibu robo tatu ya vituo vya mafuta vikiishiwa nishati hiyo au kusambaza kwa kiwango cha chini, hali ya hatari imegeukia vituo vya nguvu za Nyuklia ambavyo vinasambaza karibu theluthi tatu ya umeme nchini Ufaransa.
Kwa mujibu wa muungano wa CGT , Vituo 3 kati ya 19 vya Nyuklia vingeweka zana chini kwa maana ya uzalishaji , lakini walisema kwamba kusingeathiri upatikanaji wa umeme kwa haraka.
Mtambo wa Nogent-sur-Seine ulioko kilometa 100 kusini mashariki mwa Paris umepunguza uzalishaji wake hadi asilimia 25.
Serikali imekuwa katika shinikizo la kuangalia mikakati yake katika kipindi cha miezi minne sasa rais Francois Hollande ameahidi kuwa atafanya kila awezalo, kuhakikisha "raia wa Ufaransa na uchumi unakuwa salama."
Mtambo mmoja kati ya 8 wa kusafishia mafuta umerejea katika uzalishaji siku ya jumatano , mitambo mingine mitano bado imesimamisha au imepunguza uzalishaji.
Madereva wa magari wameonekana katika mitandao wakitafuta vituo vya mafuta ambavyo bado vina nishati hiyo.
Sera ya mageuzi
Sera ya mageuzi ya soko la ajira imetengenezwa katika namna ambayo itakuwa rahisi kwa makampuni kuajiri na kufuta wafanyakazi, ambapo makampuni kadhaa ikiwemo shirika la fedha duniani IMF linasema ni muhimu katika kuinua uchumi ulio taabani.
Hata hivyo mageuzi hayo yanapingwa na vyama vya wafanyakazi wakitaka yaondolewe kabisa kwa kuwa yanaweza kuongeza uhaba wa ajira.
Serikali ilipitisha muswada huo bungeni mwezi uliopita pasipo kupigiwa kura , hali iliyoamsha ari ya maandamano zaidi.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP
Mhariri:Yusuf Saumu