Wafanyakazi 4 wa shirika la GIZ wakamatwa Afghanistan
26 Novemba 2023Mamlaka ya Taliban nchini Afghanistan imewakamata wafanyakazi wanne wa shirika kuu la misaada linalomilikiwa na serikali ya Ujerumani, GIZ. Haya yamesemwa na wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Ujerumani.
Msemaji katika wizara hiyo amethibitisha taarifa hizo alipozungumza na shirika la habari la Associated Press, na kusema kwamba wafanyakazi wa GIZ nchini Afghanistan wako kizuizini ingawa hawajapata taarifa yoyote rasmi kuhusu kwanini wanazuiliwa.
Soma hii : Afghanistan: Nani anaruhusiwa kwenda Ujerumani?
Ameongeza kuwa wanachukulia hali hiyo kwa uzito mkubwa na kwamba wanatumia njia zote kuhakikisha kwamba wafanyakazi hao wanaachiliwa huru.
Kwa mujibu wa tovuti ya shirika hilo, GIZ inamilikiwa na serikali ya Ujerumani na kufanya shughuli zake katika takriban mataifa 120 kote duniani.
Shirika hilo hutoa miradi na huduma katika sekta za maendeleo ya kiuchumi, nishati na mazingira, amani na usalama.