Miito ya kususiwa chama cha FN
23 Machi 2015Chama cha upinzani cha kihafidhina UMP kikishirikana na waliberali wameibuka na ushindi wa duru ya kwanza ya uchaguzi wa mikoa nchini Ufaransa,wakikipiga kumbo chama cha siasa kali za mrengo wa kulia,Front National-FN,kilichokuwa kikipigiwa upatu kuwa nguvu ya kwanza ya kisiasa nchini humo.Sura hii mpya imejitokeza kukisalia miaka miwili tu kabla ya uchaguzi wa rais .
Chama cha Kisoshialisti kilichoko madarakani nchini Ufaransa na washirika wake wa mrengo wa kushoto wamepata pigo la nne baada ya lile la chaguzi za mabaraza ya miji,uchaguzi wa bunge la Ulaya na ule wa maseneta mwaka 2014.Hata hivyo kwa mtazamo jumla, wamefanya vyema kuliko ilivyokadiriwa na kujikingia kwa pamoja asili mia 28.24 za kura.
Chama cha kihafidhina cha UMP kinachoongozwa na rais wa zamani Nicolas Sarkozy na washirika wake wa kiliberali wamejikingia asili mia 32.5
Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia Front National,kilichokadiriwa na taasisi za utafiti wa maoni ya umma kingenyakua si chini ya asili mia 30 ya kura,kimejipatia asili mia 25.75.
Kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya mambo ya ndani,wagombea 220 wa mrengo wa kulia,56 wa mrengo wa kushito 8 wa FN na 6 kutoka vyama vyenginevyo,wamechaguliwa moja kwa moja katika duru hiyo ya kwanza ya uchaguzi.
Duru ya pili itafanyika jumapili Marchi 29 ijayo.Kila upande miongoni mwa vyama asilia vya kidemokrasia vya Ufaransa umepania kuwafungia njia wagombea wa chama cha siasa kali FN.
Chama cha Front National kipigwe kumbo duru ya pili
Waziri mkuu Manuel Valls amewatolea wito wafuasi wote wa vyama vya kidemokrasia,wawazuwie wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia wasipite duru ya pili."Vipigieni kura vyama vya mrengo wa kushoto au kulia ikiwa katika duru ya pili,wagombea wao watashindana na FN."Amesema.
Wito kama huo wa kukisusia chama cha siasa kali za mrengo wa kulia umetolewa pia na mwenyekiti wa UMP,rais wa zamani wa Ufaransa Nicolas Sarkozy.
Asili mia 50 tu ya wapiga kura ndio walioteremka vituoni jana.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman