1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafaransa wanaikataa katiba ya Ulaya

30 Mei 2005

Ni kizungumkuti. Wafaransa walikuwa watetezi wakakamavu kuhusu ushirikiano na Muungano wa Ulaya; lakini sasa Wafaransa hao hao, kwa kupiga kura na kuikataa katiba inayopangwa kwa ajili ya Jumuiya ya Ulaya, wameiingiza jumuiya hiyo katika mzozo mkubwa. Lakini hata ikiwa hiyo katiba haiwezi sasa kunusurika kutokana na uamuzi huo wa raia wa Ufaransa, hiyo haina maana kwamba Jumuiya ya Ulaya imefikia mwisho wake. Jumuiya hiyo itakuwa na muda kidogo wa kupumua na kuipunguza ile kasi ya kuuimarisha na kuipanua jumuiya hiyo.

Rais wa Ufaransa, Jacques Chirac, na Kansela Gerhard Schroader wa Ujerumani
Rais wa Ufaransa, Jacques Chirac, na Kansela Gerhard Schroader wa UjerumaniPicha: AP

Kwamba Wafaransa wataikataa katiba hiyo ya Jumuiya ni jambo lililotarajiwa tangu mwanzo. Kwa wiki kadhaa ilikuwa wazi kwamba mkataba huo wa kuwa na katiba ya Ulaya hautaungwa mkono na watu wengi. Wanasiasa wakubwa hapa Ulaya sasa wametahayari; hakujawekwa mpango mwengine wa mbadala pindi mkataba huo ungeshindwa kukubaliwa. Kiongozi wa sasa wa baraza la viongozi wa Jumuiya, waziri mkuu wa Luxembourg, Jean Claude Juncker, na rais wa tume ya Ulaya, Jose Barroso, jana usiku walitoa tu huko Brussels taarifa za kutojali sana juu ya kile kilichotokea. Jibu lao ni kwamba mambo yatasonga mbele kama yalivyo.

Lakini yatasonga mbele kuelekea wapi?

Wanakusudia kwamba zoezi la nchi wanachama wa Jumuiya kutoa kibali kwa katiba hiyo litaendelea hadi mwakani katika majira ya mapukutiko. Ni wakati huo ndipo wakuu wa nchi za Jumuiya watakapoamuwa cha kufanya kutokana na hali iliojiotokeza.

Na hapo tena?

Hata kama nchi zote za Jumuiya, isipokuwa Ufaransa, zitaikubali katiba hiyo, jambo ambalo halitarajiwi, itakuwa sio sawa kwa wananchi wa Ufaransa kuwaita tena wapige kura kwa ajili ya katiba ambayo haitafanyiwa mabadiliko. Haitakuwa sawa kuutumia ule mtindo kwamba Wafaransa walazimishwe kupiga kura hadi pale matokeo yatakapowafurahisha wanasiasa. Kuubadilisha mswaada huo wa katiba ni jambo lisilowezekana, kwani itabidi mpango huo wote usukwe tena upya. Hapo tena kila nchi itatoa matakwa yake na misuguano ya mashauriano yasiokwisha itafuata.

Hata kidogo haisaidii kitu kujidai kwamba mambo yatakwenda vile vile, kama yalivyo sasa. Mswaada huo wa katiba umekufa. Bila ya Ufaransa, haiwezekani Ulaya kuwa na katiba. Kura zaidi za maoni katika nchi nyingine za Jumuiya mtu anaweza kuzisahau.

Nini cha kufanya sasa?

Jee tunaweza kuiita hali hii kuwa ni mzozo, balaa au mchafukoge? Wenye kuiunga mkono katiba hiyo waliichora sura ukutani pindi wananchi watakapoikataa katiba hiyo. Lakini haifikiriwi kwamba balaa liko mbele yetu.

Kutokana na mzozo huu kunaweza kukapatikana nafasi. Hivyo. Kwa mujibu wa kamishina wa Kijerumani wa Jumuiya, Günter Verheugen, viongozi wa Jumuiya lazima wadhihirishe kwamba wanaweza kulimeza pigo hili, na, licha ya hayo, kusonga mbele. Jumuiya itaendelea kufanya kazi na haitasambaratika. Ufaransa haitojitoa kutoka kwenye jumuiya.

Hivi sasa ni muhimu kuwa na wakati wa kupumua kufikiria juu ya kasi za kuiunganisha Ulaya na kuipanua Jumuiya. Kipindi hicho cha kupumua kitachukuwa miaka mingi. Ni baada ya hapo ndipo mtu anaweza kuja tena na suala la katiba na juu ya mfumo utakaotumiwa katika kuamuwa juu ya katiba hiyo. Inawezekana kwamba makundi ya nchi yakataka kuimarisha zaidi ushirikiano wao katika masuala ya kisiasa, nje, lakini, ya mkataba wa Jumuiya. Taasisi fulani, kama vile kuwa na waziri wa pamoja wa mambo ya kigeni, inaweza ikaundwa, bila ya kuweko katiba. Haifai kuyadharau mambo mengi yaliomo katika katiba hiyo iliokufa kwa sababu tu Wafaransa wameyakataa.

Suala, kwa vyovyote, ni juu ya kuingizwa Uturuki ndani ya Jumuya. Kuna wasiwasi sasa kama mashauriano ya kuiingiza nchi hiyo ambayo yamepangwa kuanza Oktoba 3 mwaka huu yatafanyika, na kama lengo kweli litakuwa kuipatia Uturuku uwanachama kamili wa jumuiya hiyo.

Rais wa Ufaransa ambaye amedhoofika, kisiasa, kutokana na matokeo ya kura ya maoni ya jana, na Kansela Gerhard Schroader wa Ujerumani, ambaye hivi sasa naye pia ameelemewa, kisiasa, walikuwa washabiki wakubwa wa kuingizwa Uturuki katika Jumuiya. Tangu jana, Rais Chirac wa Ufaransa lazima atilie maanani kwamba siasa yake imekataliwa na watu wake. Na Kansela Schroader katika majira yajayo ya mapukutiko nafasi yake inaweza ikachukuliwa na mwanasiasa atakayeiongoza serekali ya Wa-Conservative na Waliberali ambayo itapinga kuingizwa wanachama wepya ndani ya Jumuiya.

Wapendwa Wasikilizaji, hii sio kwamba Jumuiya ya Ulaya imefikia mwisho kutokana na pigo hili la jana, lakini jumuiya hiyo itabidi ibadilike.

Miraji Othman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW