1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafaransa wapiga kura katika duru ya pili ya urais

Zainab Aziz Mhariri: Sudi Mnette
24 Aprili 2022

Raia wa Ufaransa wamepiga kura katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais siku ya Jumapili. Rais aliye madarakani Emmanuel Macron anachuana na Marine Le Pen kiongozi anayeelemea siasa za mrengo mkali wa kulia.

Präsidentschaftswahl in Frankreich
Picha: Eric Feferberg/AFP/AP/dpa/picture alliance

Uchaguzi huo wa rais nchini Ufaransa bila shaka utakuwa na athari zake katika mustakabali wa bara la Ulaya. Rais Emmanuel Macron ana kibarua kigumu katika pambano hilo dhidi ya mpinzani anayeelemea mrengo mkali wa kulia Marine Le Pen.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akipiga kura yake na pembeni mwake ni mkewe Brigitte Macron. Picha: Gonzalo Fuentes/AP/picture alliance

Macron anayeelemea siasa za mrengo wa kati anawataka wapiga kura wamchague kwa kipindi kingine cha miaka mitano licha ya utawala wake kuakabiliwa na mfululizo wa maandamano ya kumpinga, janga la corona na vita katika Ukraine. Hata hivyi iwapo Macron ataibuka mshindi basi atakuwa rais wa kwanza wa Ufaransa katika kipindi cha miaka 20 kushinda muhula wa pili.

Soma:Viongozi wa Ulaya wamuunga mkono Macron katika uchaguzi ujao

Wakati huo huo matokeo kura ya nchini Ufaransa, taifa lenye silaha za nyuklia na moja ya nchi zenye uchumi mkubwa duniani, yanaweza pia kuleta athari katika mzozo wa nchini Ukraine, wakati ambapo Ufaransa imekuwa na jukumu muhimu katika juhudi za kidiplomasia na pia ikiwa ni nchi iliyounga mkono vikwazo dhidi ya Urusi chini ya utawala wa Emmanuel Macron.

Kwa upande wake mpinzani wa Macron, bi Marine Le Pen umaarufu wake umeongezeka miongoni mwa wapiga kura wa Ufaransa. Kura za maoni zinaonyesha anamkimbiza Macron kwa kasi kuliko hapo awali.

Mgombea wa urais wa Ufaransa Marine Le Pen akitoka kupiga kura yakePicha: Yves Herman/REUTERS

Hata hivyo wengi wa wapiga kura wanaotarajiwa kumchagua Macron wanafanya hivyo ili kumzuia Le Pen kuyaendeleza mawazo yake yanayoonekana kuwa yanalemea mrengo mkali wa kulia na yanakiuka demokrasia, kama vile mpango wake wa kutaka kupiga marufuku kuvaa hijabu hadharani kwa wanawake wa Waislamu, au kutokana na uhusiano wake na Urusi.

Wagombea wote wawili katika kinyanga'anyiro hicho cha urais nchini Ufaransa wanajaribu kuzinasa kura zipatazo milioni 7.7 za wafuasi wa mgombea wa mrengo wa kushoto Jean-Luc Melenchon, aliyeshindwa katika duru ya kwanza ya uchaguzim uliofanyika mnamo Aprili 10.

Soma:Vita vya nchini Ukraine vina athari gani katika uchaguzi wa rais wa nchini Ufaransa.

Kura zote za maoni katika siku za hivi karibuni zimetabiri ushindi kuelekea kwa rais Macron mwenye umri wa miaka 44 anayeunga mkono mshikamano wa bara la Ulaya ingawa tofauti ya kura kati yake na mpinzani wake wa mrengo mkali wa kulia  Le Pen mwenye umri wa miaka 53 inaonekana wazi. Kwa sababu kura za maoni pia zinatabiri uwezekano wa idadi kubwa ya wapiga kura ambao watapiga kura zao lakini bila kuashiria waliomchagua au hata kutokupiga kura kabisa.

Baadhi ya wapiga kura nchini UfaransaPicha: Lewis Joly/AP/picture alliance

Wakati wapiga kura wa Ufaransa wanapomchagua rais siku ya Jumapili, wanakabiliwa na uamuzi wa kuchagua kati ya wagombea wawili walio na maono tofauti kwa Ufaransa ya siku za usoni.

Katika kipindi cha miaka mitano tu, Rais aliye madarakani Emmanuel Macron amepevuka kutoka kwa mwangenzi wa maswala ya kisiasa hadi kuwa kiongozi muhimu wa dunia na mtoa maamuzi mwenye uzito katika maswala ya Umoja wa Ulaya ambaye amehusika sana katika juhudi za kuvimaliza vita vya Urusi nchini Ukraine.

Soma:Macron aimarisha uongozi wake katika mjadala wa televisheni

Kiongozi wa mrengo mkali wa kulia Marine Le Pen, kwa mara ya tatu sasa anaendeleza jitihada za kuwania urais nchini Ufaransa, baba yake ndiye muanzilishi wa chama cha kupinga wahamiaji ambacho sasa anakiongoza yeye Le Pen.

Tangu kurithi uongozi wa chama hicho cha National Front mnamo mwaka 2011amesema akichaguliwa atabadilisha siasa na jamii nzima ya Ufaransa kulingana na mpango wake "Ufaransa-kwanza”.

Emmanuel Macron na mkewe Brigitte Macron baada ya kupiga kura zao Picha: Gonzalo Fuentes/AFP

Takriban wapiga kura milioni 48.8 wameandikishwa kushiriki katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais nchini Ufaransa na matokeo ya mapema yanatarajiwa kuanza nkutangazwa Jumapili usiku.

Chanzo: /AP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW