Wafaransa wapiga kura kulichagua bunge
11 Juni 2017Macron amekuwa akiogelea katika bahari ya umaarufu mwanzoni mwa utawala wake katika wiki tano tangu alipomshinda mgombea wa siasa kali za mrengo wa ulia Marine Le Pen na kuwa rais kijana kuliko wote katika historia ya ufaransa, akilitangaza baraza lake la mawaziri ambalo linavuka mipaka ya mrengo wa kushoto na kuonesha mvuto katika mikutano ya kimataifa.
Chama chake cha siasa za wastani cha Republique en Marche (Republic on the Move, REM) ama Jamhuri inayopiga hatua, chama ambacho alikiasisi mwezi Aprili, 2016 kama jukwaa lake alilotumia kuwania urais, sasa kinahitaji wingi wa kutosha katika bunge la taifa ili kumuwezesha kufanya mageuzi aliyoahidi.
Uchunguzi kadhaa wa maoni ya wapiga kura unakionesha chama cha Macron kwamba kinaweza kuchukua karibu asilimia 30 ya kura katika uchaguzi wa leo , na kukiweka katika nafasi ya mbele kabisa kuweza kupata wingi wa kutosha katika uchaguzi wa duru ya pili wiki moja ijayo. Hii inaweza kutafsiriwa kuwa ni viti 400 katika bunge lenye viti 577. Chama cha REM tayari kimepata msukumo baada ya wagombea wake kuwa wa kwanza katika majimbo 10 kati ya 11 ya nje ya nchi ambayo yamepiga kura kabla ya uchaguzi wa leo.
Wanawake wengi wamejitokeza
Jumla ya wagombea 7,882 wanagombea nchi nzima katika mchakato ambao unatarajiwa kushuhudia sura mpya zikiingia bungeni, sio kwasababu zaidi ya wabunge 200 hawagombei tena katika uchaguzi huu. Wastani wa umri wa wagombea ni miaka 48.5 na zaidi ya asilimia 42 ni wanawake.
Katika bunge lililopita wanawake walikuwa na uwakilishi wa asilimia 26.9 wa wabunge , ama jumla ya wanawake 155 katika bunge lenye viti 577, hali ambayo kwa wakati huo ni kubwa.
Iwapo hakuna mgombea atakayeshinda zaidi ya asilimia 50 katika duru ya kwanza, wawili ambao wamepata kura nyingi wanaingia katika duru ya pili, pamoja na mgombea yeyote ambaye atashinda kuwa kwa zaidi ya asilimia 12.5 za jumla ya wapiga kura katika majimbo ya uchaguzi.
Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa tangu majira ya saa mbili asubuhi kwa saa za Ulaya ya kati na vitafungwa katika miji mikubwa mnamo saa mbili usiku kwa saa za Ulaya ya kati. Zaidi ya polisi 50,000 watakuwa katika doria nchini humo ambamo bado hali ya hatari inaendelea kufuatia wimbi la mashambulizi ambayo yamewauwa zaidi ya watu 230 tangu mwaka 2015.
Ugaidi
Katika tukio la mwisho , ambalo lilifanyika Jumanne, mtu mmoja mwenye umri wa miaka 40 ambaye alijiingiza mwenyewe katika imani za itikadi kali mzaliwa wa Algeria alipigwa risasi na kujeruhiwa baada ya kumshambulia polisi kwa nyundo nje ya kanisa la mjini Paris la Notre Dame.
Akiwa amedhoofika baada ya kupata kura chache kupita ilivyotarajiwa dhidi ya mshindi wa uchaguzi nchini Ufaransa Emmanuel Macron, Marine Le Pen wa chama cha National Front anataka kujionesha kuwa chama chake ndio chama kikuu cha upinzani baada ya kupata kura milioni 10.7 katika uchaguzi wa mwezi Mei.
Macron amewapiga marufuku wagombea wote kuwaajiri ndugu zao iwapo watachaguliwa na ni lazima wafanye kazi za ushauri wakati wakiwa wabunge.
Hatua hiyo inafuatia kashfa iliyoporomosha fursa ya urais kwa mgombea wa chama cha mrengo wa kulia cha Republican , Francois Fillon, ambaye anakabiliwa na madai ya uhalifu kwa kumlipa mkewe Penelope zaidi ya euro 900,000 akimuajiri kama msaidizi wake bungeni.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / dpae
Mhariri : Bruce Amani