1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Wafuasi wa Al Sadr Iraq wavamia makaazi ya serikali Baghdad

29 Agosti 2022

Moqtada al-Sadr ajiuzulu siasa na kuibua hasira za wafuasi wake

Irak | Proteste in Bagdad | Erstürmung Regierungspalast
Picha: Hadi Mizban/AP/dpa/picture alliance

Wafuasi wenye hasira wa  ulamaa wa kidini wa madhehebu ya Shia nchini Iraq Moqtada al Sadr wamevamia makaazi ya serikali baada ya kiongozi huyo mwenye sauti kutangaza anajiuzulu siasa. Tangazo lake limekuja katika wakati ambapo mivutano imeongezeka kufuatia kiasi kipindi cha mwaka mmoja wa mkwamo wa kisiasa nchini Iraq.

Picha: Hadi Mizban/AP/dpa/picture alliance

Duru za usalama zimearifu kwamba muda mfupi baada ya Al Sadr kutoa tangazo lake hilo la ghafla,wafuasi wake waliingia kasri la serikali ambalo ni jengo la serikali lililoko kwenye eneo linalowekwa ulinzi mkali na ambako pia kuna makaazi ya ofisi za balozi mbali mbali. Wafuasi hao walivamia na kuingia hadi ndani ya kasri hilo na kukalia viti kwenye chumba inakofanyika mikutano huku wengine wakipeperusha bendera za Iraq na kujipiga picha.

Baadhi yao walijivurumisha kwenye bwawa la kuogelea kwa mujibu wa mpiga picha wa shirika la habari la AFP.Mwandishi habari wa shirika hilo ameripoti kwamba wakati maelfu ya wafuasi wengine wakisikika wakisikika wakipiga kelele kulitaja jina la Moqtada wakiwa wanaelekea kwenye eneo hilo la ulinzi mkali,jeshi kwa upande mwisngine lilitangaza amri ya watu kutotoka nje kabisa katika mji mkuu wa Iraq,Baghad kuanzia alasiri.

Picha: Hadi Mizban/AP/picture alliance

Mkwamo wa kisiasa

Ikumbukwe kwamba tangu chaguzi za bunge zilizofanyika mwezi Oktoba mwaka jana Iraq imejikuta kwenye mkwamo mkubwa wa kisiasa  ulioiacha nchi hiyo kuwa bila ya serikali mpya,wala waziri mkuu au rais kufuatia mivutano kati ya makundi yanayohasimiana  kuhusu uundaji wa serikali ya mseto. Al Sadr ulamaa anayefuatwa na mamilioni ya wafuasi na ambaye aliwahi kuongoza kundi la wanamgambo dhidi ya Marekani na vikosi vya serikali ya Iraq baada ya kuangushwa kiongozi wa zamani  Saddam Hussein  alitangaza mapema leo Jumatatu kupitia ujumbe wa Twitter kwamba anajiuzulu kwenye jukwaa la siasa.

Picha: Alaa Al-Marjani/REUTERS

Japo ni mtu aliyekuwa na mchango mkubwa katika uwanja wa siasa nchini humo hakuwahi binafsi kushiriki moja kwa moja serikalini. Kwenye tangazo lake la kujiuzulu aliongeza kusema kwamba taasisi zote zinazofungamana na vuguvugu la Sadr zitafungwa isipokuwa makumbusho ya babayake aliyeuwawa mwaka 1999 pamoja na majengo mengine ya turathi.Tamko lake hili la sasa limekuja siku mbili baada ya kusema kwamba vyama vyote Iraq ikiwemo chake vinapaswa kuachia nafasi za serikali ili kusaidia kuutatua mgogoro wa kisiasa wa miezi chungunzima.

Kundi lake la muungano wa vyama  kadhaa ndilo lililopata ushindi katika uchaguzi wa mwaka jana likinyakuwa viti 73 vya bunge lakini lilishindwa kupata wingi unaohitajika kuhodhi serikali. Mnamo mwezi Juni wabunge kadhaa kutoka mrengo wake walijiuzulu ili kutowa nafasi ya kuuondowa mkwamo lakini hatua hiyo ilipelekea kundi jingine la washia linaloegemea upande wa Iran kuwa na nguvu bungeni.

Picha: Thaier Al-Sudani/REUTERS

Tokea wakati huo Al Sadr amekuwa akitumia namna nyingine za kushinikiza ikiwemo kuitisha sala ya umma iliyowakusanya  maelfu ya wafuasi wake mnamo Agosti tano.Wafuasi wake wanataka bunge livunjwe na uchaguzi mpya uitishwe lakini pia Al Sadr amesisitiza ni muhimu vyama vyote na wanasiasa waliokuwa sehemu ya mchakato wa kisiasa tangu uvamizi wa Marekani mwaka 2003 wasishiriki tena.

Mwandishi:Saumu Mwasimba