Wafuasi wa Mursi hawataki kusalim amri
5 Julai 2013Siku mbili baada ya kumuondowa madarakani Mohammed Mursi,jeshi limetoa wito wa "suluhu ya kitaifa" na "kuepukana na kisasi " katika nchi iliyogawika vibaya sana kati ya wale wanaomuunga mkono na wengine wanaompinga Mohammed Mursi.Licha ya wito huo wafuasi wa itikadi kali wamekihujumu kituo cha polisi katika raas ya Sinai na kumuuwa mwanajeshi mmoja.
Wakijikusanya katika kile wanachokiita "Kongamano la taifa la kutetea haki" makundi makuu ya kiislamu yamewataka wafuasi wao waandamane kwa wingi na kwa amani kulaani "mapinduzi ya kijeshi.Wito huo unaonyesha kuitikwa:Katika kitongoji cha Cairo-Nasr City,maelfu ya watu wanaendelea kukusanyika,nyuso zimekunjwa,wanaonyesha mpaka leo bado hawaamini kama kiongozi wao amepinduliwa na viongozi wao wengi wamekamatwa.Si mbali na mahala waandamani hao waliko,vikosi vya usalama na vifaru vyao,vimewasimamia.
Hali kama hiyo inaonekana pia katika mji wa Mansura ambako wafuasi wa kiislam wanawatuhumu wanajeshi kutaka kuwatisha waandamanaji.Huko pia hali inatisha na waandamani wanaelezea hasira zao dhidi ya waziri wa ulinzi Abdel Fattah al Asisi.Licha ya hofu Misri isije ikatumbukia katika janga la machafuko,bado kuna wale wanaotoa wito wa utulivu :"Tutaendelea kufuata msimamo wa amani ,tutaandamana mpaka Mursi atakaporejeshwa madarakani.Naiwe leo,kesho au mwakani-tutasalia hapa hapa na hata familia zetu zitakuja kukaa huku huku".
Mashambulio yameripotiwa Sinai
Mpaka sasa hakuna machafuko yaliyoripotiwa katika uwanja wa Tahriri mji mkuu Cairo na vitongoji vyake.Kinyume lakini na katika raas ya Sinai ambako matumizi ya nguvu yameangamiza maisha ya mwanajeshi mmoja na kuwajeruhi wengine wawili.Ripoti zinasema wafuasi wa itikadi kali wamefyetua kombora na risasi dhidi ya kituo cha polisi na jeshi huko Rafah,karibu na mpaka na Gaza.Hujuma kama hizo zimeripotiwa pia dhidi ya uwanja wa ndege wa Al Arish karibu na mpaka wa Gaza na Israel.
Mwandishi:Sailer,Matthias/Hamidou Oummilkheir
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman