Wafuasi wa Raila Odinga waandamana, wawili wauawa
31 Machi 2013Muda mchache baada ya uamuzi wa majaji hao wafuasi wa waziri mkuu Raila Odinga waliandamana mjini Kisumu, Magharibi mwa Kenya kupinga uamuzi huo.
Kulingana na mwandishi habari wa shirika la AFP watu wawili walipata majeraha ya risasi katika ghasia hizo kwenye eneo hilo analotokea Raila Odinga, aliyewasilisha mahakamani kesi hiyo ya kupinga matokeo ya uchaguzi aliyosema yalikumbwa na udanganyifu mkubwa.
Kwa upande wake afisa mmoja wa polisi ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema watu wawili wameuwawa na wengine 11 wamejeruhiwa katika ghasia za hapo jana. Wakaazi wa eneo la kisumu wanasema wamekuwa wakisikia milio ya risasi usiku wa kuamkia leo na hadi wakati huu haijajulikana ni kina nani hasaa waliokuwa wanafyatua risasi hizo.
Wafuasi wa Kenyatta washerekea ushindi
Huku hayo yakiarifiwa wafuasi rais mteule Uhuru Kenyatta walimiminika jijini Nairobi wakipiga firimbi, wengine wakipiga honi za magari huku wengine wakiimba kusherehekea ushindi wa kiongozi wao.
Katika hotuba yake Kenyatta amewahimiza wakenya kuendelea kusukuma gurudumu la maendeleo ya nchi na kusema yuko tayari kufanya kazi na kuwahudumia wakenya wote bila ubaguzi.
Kenyatta mwenye umri wa miaka 51, alipata zaidi ya kura milioni 6.13, ikilinganishwa na zile za Odinga milioni 5.3. Katika uchaguzi huo wa Machi 4 kulishuhudiwa idadi kubwa ya wapiga kura katika historia ya nchi Kenya.
Takribani wakenya milioni 14.3 walijisajili kama wapiga kura na zaidi ya kura milioni 12.3 zikapigwa.
Raila akubali kushindwa
Hata hivyo Raila Odinga amekubali kushindwa na kuwatakia kila la kheri Uhuru Kenyatta na makamu wake mteule William Ruto wanapojianda kuendesha serikali mpya.
Sasa Uhuru Kenyatta ambaye ni mwanaye rais wa kwanza wa Kenya Hayati Mzee Jomo Kenyatta ataapishwa rasmi Aprili 9 kama rais wa nne wa Kenya. Kenyatta atakuwa rais wa pili barani Afrika kukabiliwa na mashtaka katika mahakama ya uhalifu wa kivita ICC.
Rais huyo mteule pamoja na mgombea wake mwenza William Ruto wote wanakabiliwa na mashtaka kuhusiana na ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007-2008 ambapo zaidi ya watu 1,200 waliuwawa huku wengine wengi hadi leo wakiachwa bila makao.
Kesi ya Ruto inatarajiwa kuanza mwezi Mei huku ya Kenyatta ikitarajiwa kuanza mwezi Julai mwaka huu.
Obama na Cameron wampongeza Uhuru
Muda mchache baada ya mahakama ya juu kutoa uamuzi wake wa kumthibitisha Uhuru Kenyatta kama rais halali wa Kenya, ofisi ya waziri mkuu wa Uingereza David Cameron, ilitoa taarifa ya kuendelea kushirikiana na Kenya.
Marekani nayo pia imetoa taarifa ya kumpongeza Kenyatta huku ikiwahimiza wakenya kudumisha amani katika kipindi hiki. Marekani pia imesifu ujasiri wa Raila Odinga kwa kukubali na kuheshimu uamuzi wa koti.
Mwandishi Amina Abubakar AP/AFP
Mhariri Iddi Ssessanga