Wafuasi wa Rais Saied waandamana Tunisia
20 Machi 2023Hayo ni baada ya ukandamizaji dhidi ya wapinzani wanaoshutumiwa kwa uhaini na rushwa na kukataa kile walichokiita uingiliaji wa kigeni. Wakiandamana katika barabara kuu ya mji mkuu, Tunis, waandamanaji hao wamesema wanataka kuisafisha nchi hiyo.
Upinzani umefanya maandamano ya mara kwa mara kumpinga Rais Saied, lakini wafuasi wake wameingia mitaani mara chache. Waandamanaji hao wamesema wanamuunga mkono Saied na kampeni yake dhidi ya wasaliti na mafisadi, dhidi ya walioiharibu nchi wakati wa muongo uliopita na wanamtaka Saied kuendeleza vita vyake bila kuchoka.
Soma pia: Mamia ya wahamiaji wa Kiafrika wenye hofu waikimbia Tunisia
Katika wiki za hivi karibuni, polisi walianzisha ukandamizaji dhidi ya makundi ya wapinzani, yanayoshutumiwa kwa mapinduzi, kuwakamata wanasiasa, viongozi wa vyama vya wafanyakazi, majaji na mfanyabiashara maarufu na mkuu wa kituo cha redio.