Wafuasi wa Ruto wahoji ushindi mkubwa wa BBI kwenye kaunti
24 Februari 2021Kufikia sasa kaunti 39 nchini Kenya zimeidhinisha mswada wa marekebisho ya katiba wa mwaka 2020, hatua inayoonekana kuupa nguvu mpango wa maridhiano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha upinzani cha ODM, Raila Odinga, licha ya madai ya hapo awali ya kukosa uungwaji mkono. Wakati hatua hii ikisherehekewa, swali linalosalia ni iwapo inalenga kumfaidisha Mkenya wa kawaida.
Kericho imekuwa kaunti ya 39 kati ya 47 zilizopitisha mswada wa marekebisho ya katiba ya mwaka 2020 mapema Jumatano. Kuidhinishwa kwa mswada huo, uliopitishwa na kaunti nyingi zaidi kinyume na ilivyotarajiwa, kumeibua maswali mapya kwenye ulingo wa kisiasa, kwani awali ilikuwa inaaminika kuwa katika maeneo ya Mlima Kenya haukuwa ukiungwa mkono.
Soma pia: BBI yapitishwa na zaidi ya kaunti 24
Kwenye mikutano yake ya umma kote nchini, Naibu Rais William Ruto amekuwa akiupinga mswada huo akiutaja kama unaolenga kuwapa uongozi matajiri na kuendelea kuwakandamiza wananchi wa chini.
Hatua ya mabunge ya kaunti kuupitisha kwa kishindo inaonekana kama pigo kubwa kwa siasa zake, ikizingatiwa kuwa eneo la Mlima Kenya na Bonde la Ufa alikojivunia ushawishi mkubwa, limeuidhinisha mswada huo. Viongozi wanaomuunga mkono wamepuuza ushindi huu.
Je, ahadi ya mikopo ya magari ndiyo iliwashawishi wawakili wa kaunti?
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii, Seneta wa Murang'a Irungu Kang'ata, ambaye awali alijiondoa kwenye kikosi cha rais baada ya kumuandikia barua akimuelezea namna BBI ilivyokosa umaarufu eneo la Mlima Kenya, anasema mswada huo umepata uungwaji mkono kwenye mabunge ya kaunti kwa sababu Rais Kenyatta aliahidi kuwapa wawakilishi ruzuku ya shilingi milioni mbili ya kununua magari.
Soma pia: Kenya kuwanunulia wawakili wa kaunti magari ya dola mil.41
Kang'ata amesema gharama zinazohitajika kutokana na kuongezwa nafasi za viongozi kama mswada huo unavyopendekeza, zitawaumiza wafanyabiashara na wakulima katika eneo lake. Mwenzake Aaron Cheruiyot, Seneta wa Kericho, anasema ushindi huo hautatatiza azma yao ya kuwapigania wananchi na kwamba BBI sio muhimu kwa sasa.
Viongozi katika kaunti zilizopitisha mswada huo wanasemekana kutia juhudi kali kuhakikisha mswada huo umepita. Wanautaja mswada huo kama mwelekeo wa siasa za taifa wakisema wanaitaka kura ya maoni ifuatie kwa haraka.
"Tunaliomba bunge liharakishe mchakato huu kwa haraka kama tulivyofanya, ndiposa tuelekee kwenye kura ya maoni. Ikija kwa watu kuamua, tuko tayari na tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha BBI inapita,” alisema gavana wa kaunti ya Migori Okoth Obado.
Mswada wa BBI, ulioasisiwa kwa azma ya kutia kikomo ghasia za kila baada ya uchaguzi mkuu pamoja na baadhi ya marekebisho ya katiba, sasa utawasilishwa kwenye mabunge ya kitaifa na seneti kabla ya kuidhinishwa na Rais Kenyatta.
Ukweli ni kuwa siasa zinaonekana kuchangia pakubwa matokeo ya mswada huo na sasa swali linalosalia ni je, kupitishwa kwa mswada huu kumewakilisha sauti ya Mkenya wa kawaida?