1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafuasi wa Azimio nchini Kenya wafanya maombolezi rasmi

26 Julai 2023

Wafuasi wa upinzani wa Azimio la Umoja leo wamefanya maombolezi rasmi kote nchini kuwakumbuka waliopoteza maisha kwenye maandamano ya wiki iliyopita

Waandamanaji jijini Nairobi nchini Kenya
Waandamanaji jijini Nairobi nchini KenyaPicha: Thomas Mukoya/REUTERS

Leo imekuwa siku ya kumbukumbu kote nchini na wafuasi wa muungano wa upinzani wa Azimio la Umoja waliositisha maandamano, wamewasha mishumaa na kufanya matembezi ya amani. Kwa hapa Nairobi, kinara wa ODM Raila Odinga aliwatembelea majeruhi wa wiki iliyopita wanaotibiwa kwenye hospitali kadhaa za jiji. Raila alisindikizwa na kiongozi wa Wiper Demokratik Kalonzo Musyoka, Eugene Wamalwa wa DAP-K, seneta wa kaunti ya Nairobi Edwin Sifuna na wengine. Akiwa Langata kwenye ibada maalum, Raila Odinga alisisitizia umuhimu wa kudumisha amani. Msafara huo wa kumbukumbu wa upinzani wa Azimio la Umoja uliwapeleka hadi hospitali za Mama Lucy Kibaki, Mbagathi na Kenyatta. Mtaani Mathare, wakazi walijitokeza nao kutoa heshima zao.

Polisi wapiga doria kwenye barabara za jiji

Katika uwanja wa Jacaranda ulioko mtaani Donholm, wafuasi wa Azimio la Umoja walijitokeza kutoa heshima zao ijapokuwa polisi walipiga doria kwenye barabara za jiji. Katika kaunti za Kisumu na Kisii, wafuasi wa Azimio walikusanyika barabarani na kuwasha mishumaa kusimama pamoja na waliopoteza jamaa zao kwenye maandamano yaliyoanza mwezi Machi mwaka huu.

Kiongozi wa Azimio La Umoja nchini Kenya - Raila OdingaPicha: Thomas Mukoya/REUTERS

Spika wa kaunti ya Kisumu Elisha Oraro aliwaongoza wakaazi walioweka maua na kuwasha mishumaa kwenye uwanja wa hospitali ya rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga.Uongozi wa Kisumu unaitolea wito serikali kufanya uchunguzi kamili wa risasi zilizotumika na kusababisha mauaji kwenye maandamano.

Ikulu ya Nairobi yajitenga na kauli za kiongozi wa upinzani Raila Odinga 

Huko Mombasa, wafuasi wa Azimio walikusanyika kwenye eneo la Pembe za ndovu kuomboleza. Yote hayo yakiendelea, ikulu ya Nairobi imejitenga na kauli za kiongozi wa upinzani Raila Odinga aliyedai kuwa rais wa nchi jirani ya Tanzania, Samia Suluhu Hassan alikuwa nchini wiki mbili zilizopita kuhudhuria kikao cha upatanishi. Kwa mujibu wa msemaji wa Ikulu ya rais Hussein Mohamed, kila rais anayeizuru Kenya rasmi hufuata taratibu maalum na wao hawakupokea taarifa za ujio huo. Ifahamike kuwa kwa sasa rais William Ruto ambaye amemnyoshea kinara wa ODM mkono wa amani yuko ziarani Tanzania kuhudhuria kikao cha maendeleo na yuko tayari kwa mazungumzo pindi atakaporejea nchini.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW