1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaripotiwa kuishambulia Syria mara 300

10 Desemba 2024

Wafuatiliaji wa masuala ya kivita wanasema Israel imefanya mashambulizi 300 dhidi ya Syria tangu kuangushwa kwa utawala wa rais Bashar al-Assad, mashambulizi hayo yameharibu miundombinu ya kijeshi.

Israel Golanhöhen Netanjahu und Katz
Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu akiarifiwa kuhusu kuimarishwa kwa vitengo vya jeshi lake kwenye mpaka wa Syria.Picha: Kobi Gideon/Israel Gpo via ZUMA Press Wire/picture alliance

Assad aliikimbia Syria huku muungano wa waasi unaoongozwa na wenye itikadi kali Jumapili iliyopitza ukiingia katika mji mkuu Damascus, na kuhitimisha miongo mitano ya utawala wa kikatili wa ukoo wa kiongozi huyo kwa kipindi chote.

Abu Mohammed al-Jolani, kiongozi wa kundi la wenye itikadi kali aliyeongoza mashambulizi yaliyomlazimisha Assad kulikimbia taifa hilo, ameanza mazungumzo juu ya uhamisho wa mamlaka na kuonesha dhamira ya kuwafuata kazi maafisa wakuu wa zamani wa serikali waliohusika na mateso na uhalifu wa kivita.

Utata wa Kundi Hayat Tahrir al-Sham na ushirikiano wa kimataifa

Kundi lake, Hayat Tahrir al-Sham, lina mizizi katika tawi la Syria la Al-Qaeda na limepigwa marufuku na serikali nyingi za Magharibi kama shirika la kigaidi, ingawa limejaribu kudhibiti mwenendo wake. Kuanguka kwa Assad, ambaye ukoo wake haukuwa na uvumilivu kwa upinzani na ambaye alidumisha mtandao tata wa magereza na vituo vya kizuizini kuliibua sherehe kote nchini Syria na ulimwenguni.

Watu huvuka kivuko kilichoharibiwa cha mpaka kati ya Lebanon na Syria ambacho kilishambuliwa na mashambulizi ya anga ya Israel, huko Arida, kaskazini mwa Lebanon,Desemba 6, 2024.Picha: AP Photo/picture alliance

Pamoja na kwamba duru zilisema kuwa Israel iliyavurumisha mamia ya makombora katika ardhi ya Syria tangu Assad alipoanza ukandamizaji wa harakati za kidemokrasia lakini kwa sasa Shirika la Uangalizi wa Haki za Binaadamu la Syria  limesema limerekodi zaidi ya mashambulizi ya 300 ya Isreal tangu kuporomoka kwa utawala wa Assad.

Viongozi wa Ujerumani na Ufaransa kufanya kazi na mamlaka mpya ya Syria

Nje ya mipaka ya taifa hilo Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na Rais wa Ufaransa Emannuel Macron wameonesha utayari wa kufanya kazi na waasi wa Syria waliompindua Assad kwa masharti fulani. Hii imebainika baada ya mazungumzo kwa njia ya simu kati ya viongozi hao wawili.

Taarifa kutoka serikalini Ujerumani ilisema viongozi wa mataifa makubwa mawili ya Umoja wa Ulaya wameipokea vyema hatua ya kuondoka kwa Assad ambaye amesababisha ile ilichokisema "mateso ya kutisha kwa watu wa Syria na uharibifu mkubwa kwa nchi yake."

Umoja wa Mataifa kupata taarifa za kina kwa uchunguzi uhalifu wa Syria

Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakikusanya ushahidi wa uhalifu uliofanywa nchini Syria nao wameonesha matumaini mapya kwamba kuanguka kwa Assad hatimaye kutamaanisha wanaweza kufikia eneo la uhalifu na kukusanya ushahidi wa kutosha.

Mwendesha mashtaka wa Canada na msomi wa sheria ambaye anaongoza chombo cha uchunguzi cha Umoja wa Mataifa kinachojulikana kama International Impartial and Independent Mechanism kuhusu Syria anasaema hatimae ushahidi utapatikana.

Soma zaidi:Israel yafanya mashambulizi makubwa nchini Syria

Rekodi zinaonesha vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria vimesababisha vifo vya watu  500,000 na kulazimisha idadi nyingine ya nusu ya nchi kukimbia makazi yao ambapo mamilioni ya hao wakipata hifadhi nje ya nchi.

Vyanzo AFP/RTR

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW