Wafugaji wataka Tanzania izuiwe kutumia ardhi
25 Januari 2022Wafugaji wa jamii ya Maasai wanaoishi katika wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha Tanzania, wamewasilisha pingamizi katika mahakama ya Afrika Mashariki wakitaka serikali ya Tanzania izuiwe kuitumia ardhi yenye kilometa za mraba 1500, kipindi ambapo mahakama hiyo bado haijatoa maamuzi ya kesi ya msingi.
Mwaka 2013, serikali ya Tanzania ilitangaza kupunguza ukubwa wa eneo la ardhi lenye kilometa za mraba 4000 hadi kufikia 1500, kwa lengo la kulinda mazalia ya wanyamapori, huku vijiji 14 vyenye wakazi takribani elfu sabini , vikiathirika kwa kukosa makazi na malisho ya mifugo.
Wananchi hao wa wilaya ya Ngorongoro mwaka 2017, walifungua kesi katika mahakama ya Afrika Mashariki wakipinga uamuzi huo wa serikali ya Tanzania kwakuwa haukua na ushirikishwaji wa wananchi, lakini kabla mahakama hiyo haijatoa uamuzi serikali imeanza kuligawa eneo hilo.
Msajili wa Mahakama ya Afrika Mashariki Yufunalis Okubo, amethibitisha kupokea maombi ya wafugaji hao ya kuitaka mahakama iweke zuio la kutumika kwa ardhi wakati kesi ikiendelea.
Veronica Natalis- Arusha