1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wagambia wapiga Kura

Admin.WagnerD1 Desemba 2016

Kura zinafanyika wakati ambapo mawasiliano muhimu ya simu kupitia mitandao ya Whattsap,Viber na Skype ikiwa imefungwa

Gambia Präsident Yahya Jammeh
Picha: picture-alliance/Landov/M. Theiler

Wananchi wa Gambia wanapiga kura katika uchaguzi wa rais ambao una ushindani mkali kati ya rais aliyeko madarakani Yahya Jameh ambaye ameitawala nchi hiyo kwa miaka 22 dhidi ya upinzani ambao umepata nguvu kubwa nchini humo. Licha ya umeme kukatika mapema leo shughuli ya kupiga kura ilianza bila matatizo katika nchi hiyo ambayo makundi ya haki za binadamu yamekuwa yakiituhumu serikali kwa kuukandamiza uhuru wa kutoa maoni.

Mshindi katika kinyang'anyiro hicho cha urais nchini Gambia kinachowakutanisha wagombea watatu atachukua uongozi wa kipindi cha muhula wa miaka mitano katika nchi hiyo ndogo iliyokuwa koloni la Muingereza katika eneo la Magharibi mwa Afrika ikipakana na Senegal.Mchezaji wa zamani wa soka  wa kimataifa kutoka Gambia Alhaji Momodo akipiga kura asubuhi  mjini Banjul amesema anamuunga mkono Jammeh kuendelea kuwa  rais kwasababu amekuwa akifanya maendeleo makubwa katika nchi hiyo, Mchezaji huyo wa zamani wa soka ameendelea kusema kwamba anaamuamini rais Jammeh na hasa kwakuwa amekula kiapo  kwa kitabu cha Quran kuitumikia Gambia na wananchi wake na kwenda kinyume na hilo mwenyezi mungu atamuadhibu.

Rais Jammeh anawania muhula wa tano madarakani  pamoja na chama chake kinachotawala cha Alliance for Patriotic Reorientation and Construction APRC:Mgombea mwingine ni aliyekuwa mbunge wa chama tawala Mama Kandeh ambaye anasimama kupitia  chama cha Democratic Congress GDC wakati mgombea wa tatu  ni mfanyabiashara asiyejulikana sana Adama Barrow ambaye anaipeperusha bendera ya muungano wa kundi la vyama vya upinzani vilivyoshirikiana mara hii kwa mara ya kwanza  na kuungwa mkono na raia wengi wa Gambia.

Waandamanaji waliokuwa wakipinga mauaji ya wapinzaniPicha: Getty Images/AFP/Stringer

Rais Jammeh ameshatoa onyo kali kwa watu watakaojitokeza mitaani kuandamana kuyapinga matokeo ya uchaguzi huo akisema hilo jambo halitokubalika.Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limewatolea mwito maafisa wa serikali kuhakikisha kwamba kipindi cha uchaguzi na baada ya mchakato huo kitakuwa na utulivu  na kuheshimiwa kikamilifu kwa haki zote za binadamu katika utoaji wa maoni yao..Inaarifiwa kwamba mawasiliano ya mtandao pamoja na simu yalizimwa katika mkesha wa uchaguzi huku mitandao mikuu ya mawasiliano kama whatsapp ,skype na Viber ikishindwa kufanya kazi.

Kutokana na hali hiyo upinzani umekuwa ukitegemea mawasiliano ya kutumiana ujumbe mfupi wa kawaida na kufanya mikutano yao pamoja na kuvuka viziuizi  vya barabarani  vilivyowekwa kila kona katika mji mkuu Banjul.

Imethibitika kwamba hakuna waangalizi wa kimataifa waliokwenda nchini humo kusimamia uchaguzi wamethibitisha pia wanadiplomasia lakini kuna kundi dogo la waangalizi wa Umoja wa Afrika pamoja na ujumbe wa Marekani na Ulaya wenye makao yake mjini Banjul.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Daniel Gakuba

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW