Wageni wazidi kuhamishwa kutoka Libya
4 Agosti 2014Meli ya Uingereza HMS Enterprise imewasili Malta leo hii ikiwa na Waingereza 110 waliohamishwa kutoka Libya ambapo mapigano kati ya makundi ya wanamgambo yanayohasimiana yamesambaa na kuingia katika mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli.
Balozi wa Uingereza nchini Libya Michael Aron amesema katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba miongoni mwa Waingereza hao walihamishwa ni pamoja na watoto 30,watoto wachanga 12 wanawake wanne wajawazito na mtu mzima mmoja na mgonjwa mmoja.Pia katika meli hiyo kulikuwa na Wajerumani na Wairish wachache.
Aron amesema wamewaondowa wananchi wao kutokana na hali kuzidi kuwa mbaya katika nchi hiyo ya Afrika Kaskazini. Wiki iliyopita Wizara ya mambo ya nje ya Uingereza imesema ubalozi wake ulioko Tripoli unahimishiwa nchini Tunisia.
Raia wa kigeni wazidi kuhamishwa
Uingereza ni mojawapo ya mataifa ya mwisho ya magharibi kutoufunga ubalozi wake Tripoli baada ya mapigano ya wiki kadhaa ya mitaani kuzilazimisha Marekani, Umoja wa Mataifa na wafanyakazi wa kidiplomasia wa Umoja wa Ulaya kuondoka nchini humo.
Meli hiyo ya Enterprise ya Uingereza ni meli ya pili kutumika kuondowa watu na familia zao kutoka Libya na kuwapeleka Malta. Meli nyengine iliyokodiwa Malta hapo Jumamosi iliwahamisha wafanyakazi 250 wa kampuni ya Hyundai kutoka Tripoli wengi wakiwa ni Wafilipino na raia wa India. Takriban wafanyakazi wengine 300 pia wamewasili Malta kwa ndege za kukodi wakitokea Libya.
Kwa upande wa kisiasa kikao rasmi cha ufunguzi wa bunge lililochaguliwa na wananchi wa Libya kilichopangwa kufanyika leo kiko mashakani kutokana Waislamu wa itikadi kali kusisitiza kifanyike Tripoli wakati wale wenye sera za utaifa wakitaka kifanyike katika mji wa mashariki wa Tobruk.
Mamlaka mbili za serikali
Bunge hilo lililochaguliwa Juni 25 lilikuwa linatazamiwa kuchukuwa nafasi ya Bunge Kuu la Taifa (GNC) lililochaguliwa kufuatia uasi wa mwaka 2011 uliomn'gowa madarakani dikteta aliyetawala kwa muda mrefu nchini humo Moamer Gaddafi.
Mwanaharakati wa kisiasa Salah al-Bakush amekaririwa akisema wako katika hali ambapo wana mamlaka mbili tafauti za serikali, bunge lilioko Tobruk na mamlaka nyengine yenye kudhibiti miji mikubwa mitatu ya Tripoli,Benghazi na Misrata ambapo zote ni ngome kuu za wapiganaji wa Kiislamu wa itikadi kali.
Mapigano mapya yamezuka hapo Jumamosi na kuuwa takriban watu 22 mjini Tripoli na kufanya idadi ya watu waliouwawa katika mji huo tokea Julai 13 kufikia 124 na kujeruhi wengine zaidi ya 500.
Hali ni mbaya Tripoli
Serikali ya mpito ya nchi hiyo imesema mamia ya familia zimepotezewa makaazi na kuna hali ya kibinaadamu inayozidi kuwa mbaya mjini Tripoli ambapo kuna uhaba mkubwa wa petroli,mitungi ya gesi na bidhaa za chakula.
Hapo jana takriban maduka na benki zote zimefungwa na anga ilikuwa imejaa moshi mweusi unaotoka kwenye bohari la mafuta lililoteketezwa na moto uliosababishwa na mapigano katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.
Ghasi hizo zinaonekana kuwa ni mapambano ya kuwania ushawishi kati ya makundi ya kimkoa na ya kisiasa wakati nchi hiyo ikitumbukia kwenye machafuko huku serikali ikishindwa kuyadhibiti makundi chungu nzima ya wanamgambo kutokana na kutokuwepo kwa jeshi madhubuti na kikosi cha polisi.
Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef