1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waghana wapiga kura kumchagua Rais

Isaac Gamba
7 Desemba 2016

Wananchi wa Ghana wanaendelea na zoezi la kupiga kura kwa ajili ya kumchagua Rais pamoja na wabunge licha ya  mashaka yaliyojitokeza juu ya uwezo wa tume ya uchaguzi nchini humo. 

Ghana Wahlen
Picha: Reuters/L. Gnago

Zoezi hilo la uchaguzi linaendelea mnamo wakati majina kadhaa  ya watu waliojiandikisha kupiga kura yakikosekana katika daftari la wapiga kura.

Licha ya mapungufu hayo maafisa wa serikali  nchini humo wametoa mwito kwa wananchi kuendelea kuwa na imani na tume ya uchaguzi nchini humo na kudumisha amani.

Ushindani mkubwa katika uchaguzi huo uko katika kinyanganyiro cha nafasi ya Rais ambapo Rais wa sasa  John Draman Mahama anachuana vikali na kiongozi mkuu wa chama cha upinzani nchini humo Nana  Akufo-Addow. Hii ni mara ya tatu mgombea huyo wa upinzani Akufo Ado kuwania nafasi hiyo baada ya kufanya hivyo katika uchaguzi wa mwaka 2008 na 2012.

Kumekuwa na kura chache za maoni  kuhusiana na uchaguzi huo lakini wachambuzi wengi wa masuala ya kisiasa  wanasema kura za nafasi ya urais zinaweza zikakaribiana kutokana na ushindani utakaonyeshwa na mgombea wa chama kikuu cha upinzani nchini humo.

Wapiga kura wana historia ya kuikataa serikali iliyoko madarakani

Rais wa Ghana John MahamaPicha: DW

Tangu mwaka 2000 wapiga kura nchini humo wamekuwa na historia ya kuikataa serikali iliyo madarakani katika taifa hilo ambalo linasifika kuendesha chaguzi zake katika mazingira ya amani.Ghana ambayo awali ilikuwa ikisifika kwa kuwa moja ya nchi zenye uchumi imara barani Afrika  imekuwa ikikabiliwa na hali mbaya ya uchumi katika miaka ya hivi karibuni  kutokana na kushuka kwa mapato yatokanayo  na mauzo yake ya dhahabu na mafuta  na hivyo kukabiliwa na hali mbaya ya uchumi iliyopelekea kuwepo kwa mfumko mkubwa wa bei.

Aidha thamani ya pesa ya nchi hiyo nayo pia ilishuka  kwa kiasi fulani tangu mwaka 2014 ingawa imeonyesha kupanda taratibu mwaka huu mnamo wakati serikali ya nchi hiyo ikichukua hatua kwa kushirikiana na  shirika la fedha la kimataifa (IMF) kwa ajili ya kufufua uchumi wa taifa hilo.

Chama tawala nchini humo cha National Democratic Congress kinasema kuwa licha ya changamoto za kiuchumi zilizopo, uchumi wa taifa hilo unatarajiwa kukuwa kwa kiwango cha asilimia 8 na kuwa serikali ya nchi hiyo tayari imeboresha miundo mbinu ya barabara pamoja na kuimarisha huduma za kijamii kama vile shule na hospitali.

 

Upinzani wailaumu serikali kwa kuchangia kuporomoka kwa uchumi

Mgombea wa upinzani Nana Akufo- AddoPicha: imago/Xinhua

Kwa upande wake chama cha upinzani nchini humo cha New Patriotic  kinasema serikali ya nchi hiyo imechangia katika kuporomoka kwa uchumi na kusababisha hali ngumu ya maisha pamoja na kuzidisha kiwango cha watu wasio na ajira.

Hayo yanatokea mnamo wakati vyombo vya usalama vikisambaza maafisa wake kote nchini ili kuimarisha ulinzi na  vyama vya siasa vikisambaza mawakala wake katika vituo 29,000 kwa ajili ya kufuatilia mwenendo wa uchaguzi huo huku pia upande wa upinzani ukisisitiza kutokuwa na imani na tume ya uchaguzi.

Mwandishi: Isaac Gamba/RTRE

Mhariri      :Yusuf Saumu

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW