1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wagombea 82 waliofutiwa matokeo wazuiwa kuondoka Kongo

9 Januari 2024

Mahakama kuu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imewazuia wagombea 82 waliofutiwa matokeo katika uchaguzi wa ubunge wa kitaifa na ule wa mikoa kuondoka nchini humo.

Mwendesha mashitaka mkuu wa Kongo apiga marufu safari za wagombea kadhaa wa uchaguzi wa bunge kwa tuhuma za rushwa
Mwendesha mashitaka mkuu wa Kongo apiga marufu safari za wagombea kadhaa wa uchaguzi wa bunge kwa tuhuma za rushwaPicha: Saleh Mwanamilongo/DW

Hayo yamejiri baada ya Tume Huru ya Uchaguzi, CENI, kufuta matokeo ya wagombea hao, wakiwemo mawaziri, magavana wa mikoa, maseneta pamoja na wabunge, kwa tuhuma za udanganyifu, ufisadi na umiliki haramu wa vifaa vya kupigia kura.

Katika barua kwa Kurugenzi Kuu ya Uhamiaji (DGM), Firmin Mvonde, ambaye ni mwendesha mashtaka mkuu, ametaka watuhumiwa hao wazuiliwe kutoka nje ya mipaka ya Kongo.  Barua nyingine ilitumwa kwa mwenyekiti wa CENI akiomba apatiwe nyaraka zote zilizompelekea kufuta matokeo ya wagombea hao.

Upande mwengine, baada ya kusikiliza hapo jana kesi kuhusu uchaguzi mkuu uliomrudisha tena madarakani Raïs Félix Tshisekedi, Mahakama ya Katiba iliomba mgombea Théodore Ngoy kutoa ushuhuda wa kutosha.

Hatua ya mahakama katika kesi hiyo inasubiriwa mwishoni mwa wiki hii.