1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Warushiana vijembe vya maneno kutetea sera za wagombea wao

5 Oktoba 2016

Mdahalo wagubikwa na vijembe kila mgombea akimkingia kifua mgombea urais wa chama chake kuelekea uchaguzi mkuu wa Novemba 8

USA Pence trifft auf Kaine - Vizekandidaten liefern sich erstes TV-Duell
Tim Kaine wa Democtrat na Mike Pence wa RepublicanPicha: Reuters/K. Lamarque

Wagombea wawili wa nafasi ya makamu wa rais nchini Marekani wameshambuliana kwa maneno makali katika mdahalo wa Televisheni kila mmoja akimshambulia mwenzake juu ya mgombea wake wa Urais na sera zao.

Ikiwa ni wiki tano kabla ya uchaguzi mkuu wagombea hao wawili wa wadhifa wa makamu wa rais kutoka chama cha Democratic Tim Kaine na Republican Mike Pence walirushiana vijembe vya maneno kuwahusu Hillary Clinton na Donald Trump huku kila mmoja lakini akijisifia uwezo alionao  ingawa pia kwa upande mwingine wakionekana kupigana vita vya maneno katika kuwakingia kifua wagombea wao wa urais kuelekea uchaguzi wa Novemba 8.

Kura za maoni zinaonesha kwamba Hillary Clinton amejiongezea umaarufu katika kipindi cha wiki iliyoonekana kama iliyompa funzo mgombea wa Republican Donald Trump ambaye amekuwa akiandamwa na utata kuhusu suala la kukwepa kodi pamoja na jinsi anavyowatendea wanawake.Seneta wa Virginia Tim Kaine ambaye ndiye  mgombea wa nafasi ya makamu wa rais wa chama cha Democtrat  alimuandama Trump tangu mwanzoni mwa mdahalo akisema fikra ya kumuunga mkono mgombea huyo kuwa amiri jeshi mkuu inawatia khofu kubwa sana.Siwezi kuamini ni vipi Gavana Pence anavyoweza kumtetea mtu kama Donuld Trump ambaye amejawa na kiburi,matusi na nadharia ya kujipendelea''ameongeza kusema Kaine.

Pence na Kaine wakipambana katika mdahalo wa TVPicha: Reuters/J. Ernst

Kadhalika mgombea huyo wa chama cha Democratic amejitapa kuwa ni mwanasiasa mwenye tajriba ya ndani ya jimbo lake, na kitaifa kwa ujumla ambaye anaweza kuwa mtu barabara wa kuwa makamu wa Clinton ambaye pia amemtaja kama mwanamke anaweza kuaminika na mwenye uwezo mkubwa wa kuwa amiri jeshi mkuu wa nchi ya Marekani.

Hata hivyo kwa upande wa mgombea wa chama cha Republican ambaye ni Gavana wa Indiana  Mike Pence aligeukia suala zima la sera za nje za Clinton akimshambulia hasa juu ya Mashariki ya kati.Alisema na hapa tunanukuu,''Tunaiona takriban nusu ya dunia nzima na hasa eneo kubwa la Mashariki ya kati likigaragara katika hali ya kushindwa kudhibitiwa.

Hali tunayoishuhudia  saa baada ya saa nchini Syria leo hii ni kutokana na  sera dhaifu za nje ambazo Hillary Clinton alisaidia kuundwa kwake na utawala uliopo sasa madarakani.Kwa Wamarekani wengi huo ulikuwa ni mjadala wa mwanzo mrefu uliowaonesha wanasiasa hao wawili ambao huenda wakajikuta katika nafasi ya kuwa  makamu wa rais  siku za usoni kwa upande utakaoshinda uchaguzi wa Novemba.Lakini pamoja na yote mwanasiasa huyo alionekana kukwepa kumtetea Trump katika masuala mengi ya utata ambayo yamekuwa yakizungumzwa na mgombea wake huyo.

Mgombea urais mwenye kauli za utata,Donald TrumpPicha: picture-alliance/dpa/J. Szenes

Pence ni mtu mtaratibu na mkimya akilinganishwa na Trump ambaye ni kiburi asiyejali na mwenye matusi wakati ambapo Kaine wa Demokrats ambaye pia ni mtulivu ameonekana kuwa mtu wa jazba kuliko Pence wakati wa mdahalo huo hasa katika kuushambulia upande pinzani.Wakati fulani alisema na hata tunanukuu,'' Donald Trump hawezi kuanzisha vita katika mtandao wa Twitter na mrembo wa taji la Miss Universe bila ya kujipiga risasi mguu wake''Kauli hiyo ililenga kutoa ujumbe kwamba Trump alipaswa kujitazama udhaifu wake kabla ya kumtusi Alicia Machado mrembo na kumfananisha na nguruwe mdogo kutokana na kunenepa  baada ya kupata taji hilo la mrembo wa dunia.Keine ana Umri wa mia 58 na Pence ana miaka 57 wote wamepishana kwa miaka 10 na wagombea wao wa urais.Kila mmoja ana mtoto anayetumikia jeshini na wote wawili wanatajwa kuwa wacha mungu na waumini wa dhati ikilinganishwa na Trump na Clinton.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW