1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wagombea sita wataka mazungumzo kabla ya uchaguzi Kongo

Saleh Mwanamilongo
1 Novemba 2023

Wagombea kadhaa wa uchaguzi wa rais wa Kongo, akiwemo Moïse Katumbi wanaitaka Tume ya Uchaguzi kuweka hadharani daftari la orodha ya wapigaji kura.

Wagombea wa urais Kongo wanatoa wito wa kuwepo kwa majadiliano ya haraka kabla ya uchaguzi kufanyika
Wagombea wa urais Kongo wanatoa wito wa kuwepo kwa majadiliano ya haraka kabla ya uchaguzi kufanyikaPicha: AFP/Getty Images, picture alliance, G. Kusema, DW

Katika taarifa ya pamoja iliyochapishwa leo mjini Kinshasa, wagombea sita wa urais wanakashifu kile wanachoeleza kuwa "ukosefu wa uwazi" katika uendeshaji wa shughuli za uchaguzi.

Moïse Katumbi, Martin Fayulu, Denis Mukwege, Franck Diongo, Josée-Marie Ifoku na Seth Kikuni wana wasiwasi  kuhusu kutokuwepo kwa uwazi katika mchakato wa ufadhili wa uchaguzi. Wagombea hawa pia wanataka mashauriano bora kati ya tume ya uchaguzi CENI na wagombeaji wote katika uchaguzi wa urais. Seth Kikuni ni mmoja wa waliotia saini tamko hilo la pamoja.

"Adui mkubwa wa mchakato wa uchaguzi ni kutoaminiana. Wahusika lazima wawe na imani ili kuwe na mchakato wa kuaminika. Tunasisitiza juu ya hili, turudi kwenye hili, na tunaomba tume ya uchaguzi Ceni watimize madai yetu. Tunachotaka ni kwamba baada ya Desemba 20, bila kujali mgombea gani atashinda, atahitaji uhalali wa kuongoza, na uhalali unatokana na uwazi wa mchakato wa uchaguzi.'', alisema Kikuni.

Wagombea hao wa urais wa Kongo pia walitoa wito kwa wapigaji kura kuwa makini na kuunda "ulinzi wa kiraia" mbele ya vituo vya kupigia kura ili kuangalia zoezi la kuhesabu kura.

Maandalizi ya uchaguzi yataendelea 

Tume ya uchagui imeidhinisha orodha ya wagombea 24 wa uchaguzi wa rais wa Desemba 20Picha: Dai Kurokawa/dpa/picture alliance

Kwa upande wake, Tume ya Uchaguzi Ceni inahakikisha kwamba mchakato wa uchaguzi utaendelea na kwamba majadiliano kwa vyovyote vile yamepangwa na wagombea wote. Didier Manara ni makamu wa pili mwenyekiti wa tume ya uchaguzi, Céni.

"Shughuli hii imepangwa ya kuweko na mashauriano kati ya Tume ya uchaguzi Céni na wagombea urais wote. Sio tu wale sita au saba waliotia saini waraka unaosambaa kwenye mitandao ya kijamii, bali watakuwa wagombea wote wa urais ambao watakutana na CENI ili tuwe na uelewa sawa katika shughuli nyinginezo za uchaguzi katika nchi yetu.'', alithibisha Manara.

Ni katika hali hii ya kutoaminiana ambapo shirika linaloshughulikia mizozo la International Crisis Group, ICG, lina wasiwasi kuhusu ghasia zinazotishia uchaguzi ujao. Katika ripoti iliyochapishwa Jumatatu, shirika hilo la kuzuia migogoro linatoa wito kwa serikali ya Kongo kuhakikisha kuwa wagombea wote wanaweza kufanya kampeni bila vikwazo.

''Tunaamini kuwa ni uchaguzi uliohatarini''

Mapigano yanaendelea jimboni Kivu ya Kaskazini baina ya jeshi na wapiganaji Maimai dhidi ya waasi wa M23 Picha: Glody Murhabazi/AFP/Getty Images

Onesphore Sematumba, mchambuzi anayehusika na nchi za Maziwa Makuu katika shirika la kimataifa la International Crisis Group , na mwandishi mwenza wa ripoti hiyo amesema kuna hatari nyingi zinazotishia uchaguzi wa Desemba.

"Tunaamini kuwa ni uchaguzi uliohatarini, ambao pia umeanza vibaya sana. Na hivyo hatari kubwa ya kwanza inahusishwa na tuhuma za kutoamaniniana. Katika ripoti yetu, tunaangazia sehemu mbili za nchi ambazo ziko katika hatari kubwa, ikiwemo Kivu Kaskazini  ambayo iko katika vita vya M23 vinavyoungwa mkono na Rwanda na kwa upande mwingine ni eneo la Katanga, huko kuna mivutano ya kikabila ambayo kwa bahati mbaya inachochewa na wanasiasa.'', alisikitika Sematumba.

Aidha ICG, imewatolea wito wadau wa kimataifa, ikiwemo mataifa yenye nguvu ya Kiafrika ambayo yana ushawishi huko Kinshasa na pia mataifa ya Magharibi, kuhimiza serikali na upinzani kufikia maelewano juu ya masuala yaliyoanishwa kuwa tayari kutoa upatanishi endapo matokeo ya uchaguzi yatapingwa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW