1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wagombea ukansela Ujerumani wachuana katika mdahalo

30 Agosti 2021

Ikiwa zimebakia wiki nne hadi kufanyika uchaguzi mkuu wa Ujerumani, wagombea watatu wanaowania kiti cha ukansela wamechuana katika mdahalo wa televisheni hapo jana Jumapili.

Deutschland | Bundestagswahl Kanzlerkandidaten Triell | Laschet, Baerbock und Scholz
Picha: Michael Kappeler/dpa Pool/dpa/picture alliance

Mada kuu zilizojadiliwa ni mgogoro wa Afghanistan, mabadiliko ya tabianchi, janga la virusi vya corona pamoja na sera za ndani ya nchi. 

Armin Laschet, kiongozi wa chama cha kihafidhina cha Christian Democratic Union (CDU), Olaf Scholz wa Social Democratic (SPD) na kiongozi wa chama cha Kijani Annalena Baerbock walishiriki katika mdahalo huo mkali wa saa mbili uliorushwa mubashara Jumapili katika vituo vya televisheni vya Ujerumani.

Soma zaidi: Je, kiongozi wa chama cha Kijani Annalena Baerbock anaweza kuwa kansela ajae wa Ujerumani?

Kutokana na mgogoro uliotokea nchini Afghanistan, kufuatia jumuiya ya kujihami NATO kuondoa wanajeshi wake nchini humo, wagombea wote watatu kwa pamoja wamesema kuna haja ya Ujerumani kuimarisha ushawishi wake kwenye suala la usalama wa kimataifa.

"Kama Wajerumani, tuna jukumu duniani; ikiwa tumeshindwa basi angalau tuwaokoe watu ambao tumewaahidi kuwaleta katika nchi iliyo salama," amesema Baerbock.

Aidha wote watatu wanapinga kutangazwa masharti zaidi yakupambana na virusi vya corona, pamoja na kwa mara nyingine tena raia kulazimishwa kusalia majumbani. Halikadhalika wagombea wote watatu wanaunga mkono kuongeza idadi ya watu waliopigwa chanjo dhidi ya virusi vya corona.

Wagombea Uansela wa Ujerumani, Laschet, Baerbock na ScholzPicha: SvenSimon/dpa/picture alliance

Chama cha SPD chaongoza

Uchunguzi wa maoni ya watazamaji uliofanywa na kituo cha televisehni cha RTL kilichorusha mdahalo huo umeonyesha kwamba Scholz ndiye mgombea aliyekubaliwa zaidi kwa asilimia 38, akimzidi kidogo Baerbock aliyepata asilimia 37, huku Laschet akishika mkia kwa asilimia 22.

Soma zaidi: Je Armin Lachet anapaswa kubebeshwa lawama za kuanguka kwa umaarufu wa chama CDU?

Kabla ya mdahalo huo wa televisheni, chama cha Scholz cha SPD kimepata umaarufu zaidi katika uchunguzi wa hivi karibuni wa maoni ya raia uliofanywa na gazeti la kila Jumapili la Bild am Sonntag. SPD kilichopata asilimia 24 kimeupita muungano wa kihafidhina unaoongozwa na Kansela Angela Merkel kwa nukta tatu.

CDU na chama ndugu cha Christian Social Union CSU kimepata asilimia 21 ya uugwaji mkono kwenye uchunguzi huo uliochapishwa Jumapili. Na chama cha Kijani kimepata asilimia 17 na kutajwa kuwa kipo katika nafasi nzuri kuweza kuunda serikali ijayo ya mseto.

Midahalo mengine miwili bado inatarajiwa kufanyika kabla ya uchaguzi wa Septemba 26 wakati Merkel atakapoachia ngazi ya ukansela.

Vyanzo: dpa,rtre, aptn