1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wagombea wa uchaguzi Kenya na kampeni za mwisho

5 Agosti 2022

Kampeni za uchaguzi mkuu nchini Kenya, zinaelekea kumalizika huku wagombea wa nyadhifa mbalimbali wakijiandaa kwa mikutano ya mwisho Jumamosi.

Kenia Wahlen 2022
Picha: Tony Karumba/AFP

Wakati huo huo, Tume ya Uchaguzi ya Kenya IEBC, imewalisha kiapo cha kutunza siri, maafisa wasimamizi wa uchaguzi huo mkuu uliopangwa kufanyika Agosti 9. Kwa upande mwengine, serikali imekanusha taarifa kuwa inapanga kuvuruga uchaguzi kwa kusitisha huduma za umeme na mtandao wa intaneti siku ya uchaguzi.

Maafisa waliokula kiapo pamoja na manaibu wao wana wajibu muhimu wa kuongoza mchakato huo kwenye vituo vya kupigia kura, wakiwa na jukumu la kuhakikisha kuwa maagizo yote yanafuatwa, kura zinalindwa na mchakato mzima unakamilika.

Mfumo wa kielektroniki kutumika

IEBC pia inajiandaa kuwapa mawakala wa wagombea wa urais ridhaa ya kuingia kwenye mfumo wa kielektroniki wa kukusanya na kurushia matokeo ya uchaguzi. Tume ya uchaguzi imeandaa mchakato wa kidijitali wa kutumia nambari au maneno ya siri kuweza kutazama matokeo kadri yanavyowasili kwenye kituo kikuu cha kuhesabia na kujumlisha kura.

Kwa upande mwengine, serikali imekanusha madai kwamba ipo njama ya kuuvuruga uchaguzi kwa kusitisha huduma za umeme wakati wananchi watakapoenda vituoni wiki ijayo. Akizungumza na waandishi wa habari, waziri wa usalama wa taifa Dokta Fred Matiangi aliuhakikishia umma kuwa huduma za umeme na mtandao wa intaneti hazitasitishwa siku ya uchaguzi.

Wafanyakazi wa Tume ya Uchaguzi wa Kenya, IEBC wakiendelea na matayarisho ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022Picha: Yasuyoshi Chiba/AFP

''Serikali haina mpango wa kuvuruga huduma zinazohitajika wakati wa uchaguzi mkuu.Kamwe hatutasitisha huduma za umeme wala mtandao,'' alifafanua Matiangi.

Kampeni za lala salama

Yote hayo yakiendelea, Ijumaa ni mkesha wa siku ya mwisho ya kampeni kabla ya uchaguzi mkuu. Wagombea wote wanajiandaa kwa mikutano ya mwisho kukutana na wapiga kura na kukifunga rasmi kipindi cha kampeni.

Muungano wa Kenya Kwanza utakutana na wapiga kura kwenye uwanja wa michezo wa Nyayo. Muda mfupi uliopita wanaogombea nafasi mbalimbali kupitia Kenya Kwanza walifika kwenye eneo la uwanja huo wa michezo kulikagua.

Kenya kwanza iko Laikipia na Nakuru kunadi sera zake. Vita vya maneno kati ya naibu rais William Ruto ambaye ni mgombea wa urais kupitia muungano wa Kenya Kwanza na Rais anayeondoka madarakani, Uhuru Kenyatta bado vinatokota.

Muungano wa Azimio la Umoja uko eneo la Pwani. Akiwa Kilifi kinara wake Raila Odinga aliwaambia wapiga kura kuwa mkombozi amefika. Wagombea wengine wawili wa urais waliosalia David Mwaure wa chama cha Agano na George Wajackoya wa chama cha Roots nao pia wanahitimisha kampeni zao.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW