1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wagombea wa Ukansela Ujerumani wachuana kwenye mdahalo

20 Septemba 2021

Wagombea watatu wa nafasi ya Ukansela nchini Ujerumani wamechuana usiku wa Jumapili kwenye mdahalo wa mwisho wa televisheni ikiwa imesalia wiki moja kabla ya uchaguzi hapo Septemba 26.

Bundestagswahl 2021 3. TV-Triell Kandidaten
Wagombea wa nafasi ya Ukansela nchini Ujerumani wakishiri mdahaloPicha: Prosieben/Seven.One/dpa/picture alliance

Wagombea hao watatu Armin Laschet wa muungano wa wahafidhina wa CDU/CSU ambao sasa ndiyo unaongoza serikali ya mseto  na Olaf Scholz kutoka chama cha SPD pamoja na Annalena Baerbock wa chama cha kijani "Die Grune" wamepambana kuhusu masuala kadhaa ikiwemo kodi, kima cha chini cha mshahara na bila shaka suala la kujenga uchumi pasi na kuharibu mazingira.

Scholz ambaye hadi sasa anaongoza kwenye uchunguzi wa maoni ya umma aliukingia kifua mpango wake kupandisha ujira kwa hadi Euro 12 kwa saa  pamoja na kuongeza kodi kwa matajiri, mkakati ambao umeshambuliwa vikali na mgombea wa CDU/CSU Armin Laschet.

Laschet ambaye anaihitaji kujiimarisha kwa alama kadhaa iwapo anataka kuongoza serikali inayokuja amesema sera ya kuongeza kodi inayopendekezwa na Scholz ni "ishara mbaya" katika wakati ulimwengu unajikongoja kurekebisha uchumi uliothiriwa na janga la virusi vya corona.

Hata hivyo Scholz ameitetea nia yake ya kuongeza ujira na kupandisha kodi kwa matajiri akisema hatua hiyo italeta nafuu kubwa kwa watu wa kipato cha chini ambao mbali ya kulipwa fedha kidogo wanaandamwa na msusuru wa makato ya kodi.

Baerbock: Enzi ya CDU/CSU imekwisha

Mgombea wa chama cha kijani Annalena Baerbock ambaye chama chake kinashika nafasi ya tatu kwenye katika uchunguzi wa maoni ya umma amepigia upat nyongeza ya marupurupu kwa wafanyakazi pamoja pia kuachana na matumizi ya makaa ya mawe katika uzalishaji nishati akisema serikali ijayo nchini Ujerumani ni lazima iwe inayojali mazingira.

Ingawa ulikuwa mdahalo mrefu uliojadili masuala mazito kuelekea uchaguzi, mtu angeweza kusema umesaidia pakubwa walau kuchora picha halisi ya nani anabeba turufu ya ushindi mnamo Septemba 26

Kwa jumla wale waliofuatilia mdahalo huo wanaweza kuhitimisha kwamba ilikuwa ni Scholz aliyejiunga na Baerbock kumkaba koo Bw. Laschet wakizishambulia sera za muungano wa vyama ndugu vya kihafidhina na hata kwenda umbali wa kusema miaka 16 ya utawala wa CDU/CSU imetosha na muda umewadia kuhamia upande wa upinzani.

Na aliyepigilia msumari wa mwisho hoja hiyo alikuwa bibi Baerbock wa chama cha kijani "Nimelieleza hili wazi wazi kwamba ninadhani ni muda mwafaka kwa muungano huu kuhamia upinzani. Sisi na SPD tunakubaliana kwenye maeneo mengi ya sera za jamii, lakini kama nilivyosema, tunahitaji chama imara cha kijani  juu ya wote ili kuanza upya vizuri"

Scholz awavutia watazamaji wa mdahalo 

Maoni yaliyokusanywa baada ya mdahalo huo yanaonesha Scholz alifanya vizuri jukwaani akijikingia asilimia 42 ya kura za watazamaji huku Laschet akaimbulia asilimia 27 na kufuatiwa na Baerbock aliyewavutia wafuatiliaji kwa asilimia 25.

Picha: Arne Dedert/dpa/picture alliance

Wakati hayo yakijiri Scholz ambaye sasa ni waziri wa fedha wa Ujerumani leo ameitwa kwenye kikao maalum mbele ya kamati ya bunge kuhojiwa kuhusu matukio kadhaa yanayohusishwa na utakatishaji fedha yaliyofanywa na ofisi moja ya forodha iliyo chini ya wizara yake. Wengi wanatilia shaka kwamba uamuzi wa kuanzisha uchunguzi huo sasa unamlenga mwanasiasa huyo kuelekea uchaguzi unaokuja.

Mhariri:Yusuf Saumu

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW