Wapinzani Kongo kufanya maandamano kupinga uchaguzi
23 Desemba 2023Kwa mujibu wa Jean-Marc Kabunda, mwakilishi wa mgombea Martin Fayulu, wanasiasa hao wamewasilisha barua kwa gavana wa jiji la Kinshasa siku ya Jumamosi.
Kabunda amesema barua hiyo inaelezea azma ya maandamano hayo ambayo ni ya kupinga ukiukwaji uliojitokeza wakati wa kupiga kura na kabla ya zoezi la kupiga kura na kuongezwa zoezi la kupiga kura kwa siku moja zaidi.
Soma Pia:Kongo yaanza kutangaza matokeo ya awali ya uchaguzi
Mwakilishi wa mgombea Martin Fayulu amesema kasoro zilizotajwa kwenye barua hiyo ni za kutosha kuona kwamba mnamo Desemba 20, 2023, uchaguzi wa nchini Kongo ulikuwa wa udanganyifu.
Tume ya uchaguzi nchini Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo, CENI, imekiri kuchelewa kuanza shughuli za kupiga kura mnamo Desemba 20 ambapo haikuwezekana kwa baadhi ya vituo kufunguliwa lakini tume hiyo ya uchaguzi imeyakanusha madai ya kufanyika udanganyifu katika uchaguzi huo kwa kuongeza muda wa kupiga kura.
Katika kikao cha waandishi habari katika mji mkuu Kinshasa, Rais wa CENI Denis Kadima kwa mara nyingine alipinga ukosoaji wa upinzani na waangalizi huru kuwa uchaguzi huo uliorefushwa ulikuwa na vurugu na ulikosa uhalali.
Soma Pia:Kwa nini uchaguzi ni muhimu DR Kongo?
Matokeo ya awali ya uchaguzi wa urais nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yalianza kutolewa tangu siku ya Ijumaa huku matokeo kamili ya awali ya uchaguzi huo yakiwa yanatarajiwa kutolewa mnamo Desemba 31.
Rais Felix Tshisekedi anayewania muhula wa pili madarakani alikabiliana na wagombea wengine 18 wa upinzani kwenye kinyang'anyiro cha urais. Matokeo ya awali kutoka kwa maelfu ya wapiga kura wa jamii ya Wakongo walioko nje ya nchi yanaonyesha, Rais Felix Tshisekedi anaongoza dhidi ya wapinzani wake.
Matokeo hayo ni kutoka kwa raia wanaoishi Afrika Kusini, Ubelgiji, Ufaransa, Canada na Marekani.
Vyanzo: RTRE/AFP