1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wagombea wa urais Congo kuwasilisha nyaraka zao

5 Agosti 2018

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inaanza wiki muhimu, ambapo Rais Joseph Kabila anatarajiwa kutangaza kama atawania tena katika uchaguzi baada ya mgombea mmoja mkuu kurejea nyumbani na mwingine kuzuiwa kuingia Congo

Kongo Ankunft Oppositionsführer Jean-Pierre Bemba
Picha: Reuters/K. Katombe

Jamhuri ya Kideomkrasia ya Congo ilitumbukia katika mgogoro karibu miaka miwili iliyopita baada ya Kabila kukataa kujiuzulu. Na imeendelea kuchafuka Zaidi kutokana na kurejea kwa aliyekuwa makamu wa rais Jean-Pierre Bemba, mwenye umri wa miaka 55, ambaye alifutiwa mashitaka ya uhalifu wa kivita mjini The Hague, na kurejea Kinshasa kwa ziara fupi ya kuwasilisha nyaraka zake za kugombea uchaguzi wa Desemba 23. Anatarajiwa kurudi Ulaya wiki hii.

Mgombea mwingine ni Moise Katumbi, gavana wa zamani maarufu wa mkoa wenye utajiri wa madini Katanga – ambaye amekuwa akiishi uhamishoni baada ya kutofautiana na Kabila.

Kabila anatarajiwa kutangaza msimamoPicha: Getty Images/AFP/T. Nicolon

Lakini wafuasi wake wamekasirishwa baada ya maafisa kumzuia mara mbili kurejea nyumbani, na wakasema anaweza kukamatwa kama atakanyaga nchini humo.

Georges Kapiamba, wakili wa haki za binaadamu na Rais wa chama cha Kupatikana Haki nchini Congo anasema Katumbi anaonekana kuwa mgombea mkuu kwa sababu anatokea Mashariki mwa nchi, kama tu Kabila, na anaweza kupata uungwaji mkono katika eneo hilo.

Anasema Katumbi, mwenye umri wa miaka 53, anaweza kuungana na kiongozi mwingine mkuu wa kisiasa, Felix Tshisekedi mwenye umri wa miaka 55 – muungano ambao unaweza kuwa kitisho kikubwa kwa Kabila au mrithi wake atakayechaguliwa.

Wakati muda wa mwisho wa Jumatano usiku ukikaribia, kuna hofu inayoongezeka kuwa Kabila, mwenye umri wa miaka 47, huenda akadai kuwa amekamilisha muhula mmoja pekee chini ya katiba iliyorekebishwa na kugombea tena.

Ida Swayer, mkurugenzi wa shirika la Human Rights Watch kanda ya Afrika ya Kati anasema kwa kufanya hivyo kutaongeza kitisho cha kuzuka machafuko makubwa na ukosefu wa utulivu ambapo kutakuwa na uwezekano wa kutokea madhara makubwa katika kanda hiyo.

Katumbi na Bemba ni wagombea wengine wakuu

Lakini mchambuzi wa siasa nchini Congo Jean-Claude Mputu anasema bado kuna uwezekano kuwa anaweza kumchagua mrithi wake, anafahamu kuwa hatohitajika kugombea tena.

Kama itakuwa Kabila au mrithi wake atakayemchagua mwenyewe ambaye atagombea, upinzani utahitajika kuungana wakati Desemba ikikaribia – jukumu ambalo litawahitaji wagombea kuweka kando tofauti zao za kisera au za kibinafsi na kuwahimiza wafuasi wao kufikia maelewano.

Paul Fagan, mkurugenzi mkuu wa mipango ya haki za binaadamu na demokrasia katika taasisi ya McCain ya masuala ya uongozi wa kimataifa katika Chuo Kikuu cha Arizona amesema uchaguzi huu utakuwa na ushindani mkubwa sana.

Kama kuna wagombea kadhaa wakuu kama vile Jean-Pierre Bemba, Moise Katumbi, Felix Tshisekedi, Vital Kamerhe na Joseph Kabila, basi mambo yatamuendea vyema Kabila au mrithi atakayemchagua kwa sababu wagombea wa upinzani watazigawa kura.

Katika utafuti wa karibuni wa maoni uliofanywa kwa pamoja na mashirika ya CRG/BERCI, Katumbi na Tshisekedi walitoshana kwa asilimia 19 ya kura kote nchini. Bemba alipata asilimia 17 na Kabila akapata asilimia 9. Karibu asilimia 62 haiiamini tume ya taifa ya uchaguzi CENI kuandaa uchaguzi wa huru na haki.

Mwandishi: Bruce Amani/AFPE
Mhariri: Yusra Buwayhid

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW