1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wagombea wanawake Kenya walia na vitisho

Sylvia Mwehozi
17 Mei 2017

Serikali ya Kenya inapaswa kuwalinda wanasiasa wanawake dhidi ya unyanyasaji, vipigo na vitisho wakati huu ambapo taifa hilo linaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwezi Agosti.

Kenia Frauen Politik 2007
Picha: Roberto Schmidt/AFP/Getty Images

Hayo ni kwa mujibu wa wagombea wanawake kufuatia mashambulizi kadhaa na kifo cha mtu mmoja kinachohusishwa na uchaguzi huu. 

"Hatari wanayokutana nayo wagombea wanawake haikubaliki na imevumiliwa kwa muda mrefu", ndivyo anavyoanza kwa kusema Esther Passaris ambaye alikuwa akilengwa wakati wa kampeni zake mwishoni mwa juma katika moja ya viti pekee vya wanawake  nchini Kenya.

Passaris alifungiwa kwenye chumba katika chuo kikuu cha Nairobi siku ya Jumamosi na kundi la wanaume walokuwa wakihitaji kiasi ya shilingi  za Kenya laki 150,000 sawa na dola 1450 ili kumruhusu kufanya mkutano wake uliopangwa. Kwa bahati nzuri mlango ulifunguliwa baada ya wafuasi wake kuwashinda wale wa mpinzani wake.

Kenya imetengeneza jumla ya viti 47 vya uwakilishi wa wanawake mwaka 2013 ili kuongeza idadi ya wanawake bungeni.

Nchi hiyo ndiyo yenye idadi ndogo ya wanawake bungeni Afrika Mashariki kwa asilimia 19 na wanawake wamehangaika kupata nafasi huku wakikabiliwa na vurugu, vitisho na ubaguzi wa kijinsia.

Wanawake wa Kenya wakiimba kumkaribisha Rais Uhuru KenyattaPicha: Reuters/Noor Khamis

Wakati wa kura za mchujo mwezi uliopita zilizotawaliwa na fujo, mlinzi wa mbunge Millie Odhiambo kwa jimbo la Mbita magharibi mwa Kenya aligongwa na kuuawa na gari ya upinzani. Siku chache baadae nyumba yake ilichomwa moto.

Josephine Mongare aliye mwenyekiti wa chama cha wanawake mawakili FIDA anasema wameshangazwa na namna polisi isivyoshughulikia vurugu hizo. " Hawaonyeshi hali yoyote ya udharura kwa vurugu hizi dhidi ya wanawake ambazo zimesababisha vifo na kutishia kutokea kwa wanawake zaidi", alisema Josephine Mongore.

Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya nchi Mwenda Njoka anasema wanawake si waathirika pekee wa vurugu za kisiasa, na kuongeza kwamba jeshi la polisi haliwezi kuwa na kikosi maalumu kwa ajili ya kundi fulani la wagombea iwe wanawake ama wanaume akiwataka kubeba jukumu wao wenyewe la usalama na kuepuka kuwachokoza wapinzani wao.

Hata hivyo wagombea wanawake walishambuliwa wazi katika kura za mchujo, tume ya taifa ya haki za binadamu ilisema siku ya jumatatu, ikiwa ni pamoja na mashambulizi , vitisho vya vifo na kuwachomea mali zao.

Ilitoa wito kwa serikali kuwaondolea usajili wagombea na vyama vilivyohusika katika vurugu hizo. Kenya imewafungulia mashitaka jumla ya watu 62 mwezi huu katika kesi zinazohusu mchakato wa kura za mchujo ikiwa ni pamoja na kuwahonga wapiga kura na kuchochea vurugu.

Sarah Korere ni mbunge wa sasa katika jimbo la kaskazini la Laikipia, anasimulia namna alivyoibiwa baadhi ya vitu katika gari yake mwezi uliopita wakati wa kampeni. "Kulikuwa na jumla ya magari matatu ya vijana na walevi wakisema kwamba hawawezi kukubali mwanamke awahutubie".

Wanawake wa kimasai nchini Kenya wakiwa tayari kupiga kura huko KumpaPicha: picture-alliance/AP

Korere anasema tangu alipokuwa mbunge mwaka 2013, amedharauliwa na kuitwa malaya wakati wa mikutano ya hadhara na kulaaniwa na wazee.

"Walikuwa wananigopesha mno lakini kutokana na muda nimejifunza kutowajali", anasema Korere akiongeza kwamba huwalipa wanaume karibu 100 kumsindikiza katika matukio ya hadhara akiwemo pia mlinzi wake aliye na silaha.

Wanawake hao wanasema kwa hivi sasa wamezoea hali hiyo na wamejifunza kukabiliana na hilo, hasa wanapoona kwamba wanawake wanasiasa wanapata umati mkubwa wa watu zaidi yao kisha hapo wanaacha vitendo hivyo.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/Thomson Reuters Foundation

Mhariri: Saumu Mwasimba

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW