1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wagombea wanawake ni wachache uchaguzi wa DRC - CAFCO

19 Oktoba 2023

Muungano wa mashirika ya wanawake nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (CAFCO) umeelezea kusikitishwa na idadi ndogo ya wanawake waliokubaliwa kugombea katika uchaguzi mkuu wa Disemba 20.

Demokratische Republik Kongo | symbolisches Wahllokal in Beni
Harakati za uchaguzi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Picha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inatarajiwa kufanya chaguzi nne mnamo Desemba 20, ukiwemo wa rais, wabunge wa kitaifa na mikoa, pamoja na chaguzi za manispaa.

Lakini idadi ya wanawake waliokubaliwa kuwa wagombea kwenye ngazi hizo nne ni ndogo sana. Ni mwanamke mmoja tu kati ya wagombea 24 kwenye orodha ya muda ya uchaguzi wa urais.

Soma zaidi: Mkuu wa zamani wa polisi DRC atishia mapinduzi

"Licha ya kuwa sheria ya uchaguzi inasema kwamba vyama au vikundi vya kisiasa vinavyowasilisha asilimia 50 ya wanawake havitalipa  ada ya kugombea, kwa bahati mbaya tumegundua kwa uchungu kwamba wanaume walipendelea kulipa ada na sio kuwepo  wanawake."

Alisema Viviane Kitete, mmoja wa wasemaji wa CAFCO, kwenye mkutano ulioandaliwa na jumuiya hiyo jijini Kinshasa kutathmini mchango wa wanawake kwenye uchaguzi huo wa Disemba 20.

Kitete alisema "kwa bahati mbaya ni mwanamke ndiye anayepoteza."

Kongo inawahitaji wanawake kwenye uongozi

Hayo yanajiri huku Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikihitaji mabadiliko, ambayo yangelichangiwa na "kuwepo kwa idadi kubwa ya wanawake kwenye ngazi za uwajibikaji," kwa mujibu wa Enock Ngila, kiongozi wa Chama cha Demokrasia kwa Wote, ambaye pia alishiriki mkutano huo. 

Baadhi ya wanawake mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwenye shughuli zao za maendeleo.Picha: Paul Lorgerie/DW

"Unajua, wanawake ni viumbe ambao kwa asili wana upande wa ulinzi, ujamii na udhibiti. Ni viumbe wenye uwezo wa kuleta mitazamo mingine ya kisiasa, kijamii, kiuchumi, kijeshi na nyinginezo. Kongo inahitaji mabadiliko na itikadi hii ndiyo italeta mabadiliko. Mabadiliko nchini Kongo yatategemea kuwepo kwa wanawake kwenye ngazi za uwajibikaji." Alisema.

Soma zaidi: Tshisekedi amtaja Kagame "adui" wa Kongo

Akiwa ziarani mjini Bunia katika mkoa wa Ituri, Rais Félix Tshisekedi akisisitiza mnamo Juni 2021,  kwamba anataka mrithi wake awe mwanamke.

Ikiwa hilo litawezekana ama la, ni suala la kungoja na kuona.

Imetayarishwa na Jean Noël Ba-Mweze/DW Kinshasa

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW