1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wagombea washiriki mdahalo wa mwisho Ujerumani

24 Septemba 2021

Wagombea kutoka vyama vyote saba vikuu kwenye uchaguzi wa Ujerumani wameshiriki mdahalo wa mwisho wa televisheni usiku wa kuamkia Ijumaa.

ARD Schlussrunde I Wahlen 2021
Picha: Tobias Schwarz/POOL/AFP/Getty Images

Mdahalo huo umefanyika huku zikiwa zimesalia siku tatu tu kabla ya uchaguzi ambao utabiri wa atakayeushinda, bado ni kitendawili.

Mdahalo wa Jumatano ulikuwa tofauti na mingine iliyopita ambapo wagombea wote saba walialikwa kinyume na watatu kutoka vyama vikuu kama ilivyokuwa awali.

Mabadiliko ya tabia nchi ni hoja iliyojadiliwa kwa kina

Annalena Baerbock wa chama cha Kijani, Olaf Scholz wa chama cha Kisoshalisti cha SPD, Armin Laschet wa chama cha Christian Democratic Union CDU, waliungana na wenzao Christian Lindner wa Free Democrats FDP, Markus Söder wa chama cha CSU na Alice Weidel wa chama cha AfD pamoja na Janine Wissler wa chama cha siasa za mrengo wa kushoto.

Armin Laschet wa chama cha CDUPicha: Clemens Bilan/Pool/Getty Images

Mojawapo ya hoja zilizopewa uzito kwenye mdahalo huo ilikuwani mabadiliko ya tabia nchi. Lakini badala ya kuzungumzia suala zima la mabadiliko ya tabia nchi kwa ujumla, wagombea walizungumzia hatua binafsi walizochukua ili kupunguza uchafuzi wa mazingira.

Kwa mfano Laschet alisema kwamba anaendesha gari linalotumia umeme na anafurahia, huku Söder akidai kwa sasa amepunguza kiasi cha nyama anachokula kwa ajili ya kuhifadhi mazingira. Annalena Baerbock naye alisema kwamba amekuwa akitumia basi kwa usafiri badala ya ndege katika wiki zake saba za kampeni.

Mdahalo wa JUmatano ndio uliokuwa wa kwanza kutoa muda mrefu katika kujadili masuala ya sera za kigeni. Mgawanyiko ulikuwa wazi miongoni mwa wagombea katika suala la matumizi ya ulinzi na lengo la muungano wa kujihami wa NATO la asilimia mbili ya pato jumla.

Mradi wa gesi wa Nordstream 2 bado una utata

Waziri wa fedha Olaf Scholz alisema kuna haja ya kutumia fedha zaidi katika ulinzi ila kwa uzingativu wa hali halisi ya kiuchumi lakini Wissler alipinga moja kwa moja akisema matumizi ya fedha nyingi katika ununuzi wa silaha hayatoufanya ulimwengu kuwa mahali salama pa kuishi. Wissler akidai kuna sehemu nyingi muhimu ambapo fedha hizo zinahitajika kutumika.

Armin Laschet wa chama cha CDU aliulizwa iwapo anataka mradi wa gesi wa Nordstream 2 kutoka Urusi hadi Ujerumani uanze na alikuwa na haya ya kusema.

"Ndio, tunahitaji mradi huu wa kiuchumi kwa sababu tukiacha matumizi ya vyanzo vyengine vyote vya nishati, bila shaka tutahitaji gesi katika miaka michache ijayo. Kwangu mimi ni muhimu kwamba kile ambacho serikali ya Ujerumani imekubali, kianze kutekelezwa," alisema Laschet.

Mradi wa Nordstream 2 umekuwa ni suala lenye utata hasa kwa nchi za mashariki mwa Ulaya pamoja na Marekani.

Annalena Baerbock wa chama cha KijaniPicha: Clemens Bilan/Pool/Getty Images

Mdahalo huu umefanyika huku kura ya mwisho ya maoniikionyesha ushindani ukiwa mkali mno huku chama cha SPD kikiwa na asilimia 25 nacho chama cha Kihafidhina cha CDU na chama chake ndugu cha CSU vikiwa na asilimia 23 huku chama cha kijani kikiwa katika nafasi ya tatu kwa asilimia 16.5.

Hii inamaanisha kwamba kutakuwa na majadiliano marefu na kutoelewana kwingi kabla serikali kuundwa baada ya uchaguzi.

Huku hayo yakiarifiwa, wagombea wote IJumaa wanaingia katika duru ya mwisho wa kampeni huku vyama vyao vikiwa vinaelekea kukamilisha machakato huo wa kusaka kura kuelekea uchaguzi wa Jumapili.

Vyanzo: dpa/ https://bit.ly/3i3f4fj