Wagombea wawili kuchuana duru ya pili ya uchaguzi Sri Lanka
22 Septemba 2024Mgombea anayeegemea upande wa siasa za kijamaa nchini Sri Lanka Anura Kumara Dissanayake na kiongozi wa upinzani Sajith Premadasa watachuana katika duru ya pili ya uchaguzi wa uraiskulingana na tume ya uchaguzi.
Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Sri Lanka kwa kinyang'anyiro cha urais kuamuliwa kwa duru ya pili ya kuhesabu kura baada ya wagombeaji wawili wa juu kushindwa kupata asilimia 50 ya kura zinazohitajika ili kutangazwa mshindi.
Soma: Raia wa Sri Lanka wapiga kura ya kumchagua rais
Tume ya uchaguzi imewaeleza waandishi wa habari kwamba wagombea wote waliosalia, akiwemo Rais aliye madarakani Ranil Wickremesinghe, wameondolewa. Dissanayake amepata asilimia 39.5 ya kura zilizohesabiwa huku Premadasa akimaliza nafasi ya pili kwa asilimia 34. Wickremesinghe, ambaye aliongoza taifa hilo lililokuwa na madeni mengi ameshika nafasi ya tatu kwa asilimia 17.