1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Wagombea wawili kuchuwana na Assad uchaguzi Syria

3 Mei 2021

Mahakama ya Juu ya Kikatiba nchini Syria imewapitisha wagombea wawili kushindana na Rais Bashar al-Assad katika uchaguzi ambao mataifa ya Magharibi yanasema utaathiri juhudi za kidiplomasia kukomesha vita.

Syrien Wahl 2021 | Bashar al Assad
Picha: Syrian Presidency Facebook page/AFP

Mkuu wa mahakama hiyo, Mohammed Jihad al-Lahham, aliwaambia waandishi wa habari siku ya Jumatatu (Mei 3) kwamba mahakama imeyakubali maombi ya watatu hao, na kuyatupilia mbali ya wengine 48, ambao wamepewa nafasi ya kukata rufaa ndani ya kipindi cha siku tatu.

"Kwa mujibu wa muda waliowasilisha maombi yao na kumbukumbu kwenye majalada ya Mahakama ya Juu ya Katiba, maombi ya kugombea ya kwanza: Abdallah Saloum Abdallah, pili: Bashar Hafez al-Assad, tatu: Mahmoud Ahmed Marei, wamethibitishwa, huku maombi yaliyobakia yamekataliwa kwa sababu ya kukiuka masharti ya kikatiba na kisheria." Alisema mkuu huyo wa mahakama.

Marai ni miongoni mwa wapinzani wachache wanaovumiliwa na Assad na anaishi mjini Damascus, anakoongoza chama kidogo cha siasa.

Abdallah ni waziri wa zamani wa masuala ya bunge na pia mbunge. 

Assad, aliyeingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 2000, anatazamiwa kushinda tena kirahisi uchaguzi huo.

Mara ya mwisho alichaguliwa tena kushika wadhifa huo kwa muhula wa miaka saba mwaka 2014. 

Mbali na kukosa upinzani wa maana dhidi yake, Assad amefanikiwa kurejesha udhibiti wa sehemu kubwa ya Syia, miaka 10 baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kuangamiza maisha ya maelfu ya watu na kuwageuza mamilioni kuwa wakimbizi.

Umoja wa Mataifa wakosowa uchaguzi

Kwa mtazamo wa Damascus, uchaguzi ni mfumo unaofanya kazi licha ya taifa hilo kuwa vitani.

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria, Geir Pedersen.Picha: Louai Beshara/AFP

Lakini upinzani na mataifa ya Magharibi yanauona kama kituko kinachokusudiwa kumuweka Assad madarakani milele na kuyauwa majadiliano ya kuumaliza mgogoro uliopo.

Maafisa wa juu wa Umoja wa Mataifa walisema mwezi huu kwamba kura hiyo haitokidhi matakwa Baraza la Usalama linalotaka mchakato wa kisiasa kuumaliza mgogoro wa Syria, katiba mpya na uchaguzi huru chini ya uangalizi wa Umoja wa Mataifa.

Katika siku za hivi karibuni, Assad amechukuwa hatua kadhaa kupunguza hasira za umma kutokana na kuporomoka hali ya maisha na thamani ya sarafu ya nchi hiyo, kwa kupandisha mishahara, kuwaandama walanguzi na kurejesha hadhi ya sarafu katika kiwango cha soko lisilo rasmi. 

Hata hivyo, wakosoaji wake wanasema baadhi ya hatua alizochukuwa, kama mikopo ya masharti nafuu, zinawapendelea kiuchumi na kisiasa washirika wake wakuu, hasa ndugu zake wa jamii ya wachache kutoka madhehebu ya Alawi, ambao ndio walio wengi kwenye serikali na vyombo vya usalama. 

Siku ya Jumapili, Assad alitangaza msamaha kwa baadhi ya walanguzi, wacheza kamari na wahalifu wa makosa madogo madogo, hatua ambayo ndugu na jamaa wanategemea itasababisha kufunguliwa kwa baadhi ya wanaharakati wa kijamii waliotiwa nguvuni hivi karibuni.

Mgogoro wa Syria ulianza kama maandamano ya amani kudai hali nzuri zaidi za maisha na sheria mwezi Machi 2011, lakini baada ya serikali kuchukuwa hatua za kikatili kuwaangamiza waandamanaji, ukageuka kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea hadi sasa.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW