Ghana: Maombi badala ya tiba kwa wagonjwa wa akili
27 Januari 2026
Ilikuwa ni Ijumaa asubuhi katika Msitu wa Achimota, eneo la kijani katikati ya mji wa Accra, ambako makundi ya waumini walikuwa wakimiminika kwa wingi kuomba. Msitu huo umegeuka kuwa hifadhi isiyo rasmi kwa familia zilizokata tamaa kutafuta uponyaji wa matatizo ya akili.
Kutoka nje, bustani hiyo na bustani ya wanyama ya Accra Zoo zilionekana tulivu, matawi yakitikiswa na upepo mkavu. Ndani zaidi, sauti za maombi zilipanda, baadhi ya waumini wakizungumza kwa lugha za ndimi na wengine wakianguka chini kana kwamba wameshikwa na nguvu zisizoonekana.
Katika uwazi mmoja wa msitu, aliketi mwanamke mwenye umri wa miaka thelathini hivi, akiwa mchafu na macho yake yakitazama pasipo lengo. Alionekana kama aliyekata tamaa kabisa.
Familia yake ilisema alipata "usumbufu wa akili” mwezi mmoja uliopita. Walimleta kwa Nabii Elisha Ankrah wa Kanisa la The World for Christ, wakiamini mateso yake ni ya kiroho na si ya kitabibu.
"Kile ambacho madaktari wanashindwa, Mungu anaweza,” alisema Ankrah, akiwa amevaa mavazi meupe. "Wengi huja hapa baada ya hospitali kushindwa. Kupitia maombi na kufunga, wanapona.”
Msongamano wa imani na uhaba wa huduma
Mandhari kama hayo yamekuwa ya kawaida kote Ghana, wakati mwingine yakimalizika kwa madhara makubwa. Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema msongo wa mawazo na wasiwasi vimeongezeka baada ya janga la Covid-19 barani Afrika.
Nchini Ghana, zaidi kidogo ya wataalamu 80 wa magonjwa ya akili wanahudumia watu zaidi ya milioni 35, kulingana na Mamlaka ya Afya ya Akili (MHA). Huduma za kitabibu ni haba sana nje ya miji mikubwa.
Ingawa zaidi ya asilimia 21 ya Waghana wanaishi na matatizo ya akili ya kiwango cha kati hadi kikubwa, ni asilimia mbili pekee ya bajeti ya afya inayotengwa kwa afya ya akili. Hali hiyo imeziacha familia nyingi bila chaguo.
Kwa sababu hiyo, familia nyingi hukimbilia kambi za maombi misituni na waganga wa kiroho, wakisukumwa na imani kwamba magonjwa ya akili husababishwa na laana, uchawi au mapepo.
Roho dhidi ya tiba
Umbali wa takribani saa moja na nusu, katika Kambi ya Maombi ya Mount Horeb huko Mamfe, Mkoa wa Mashariki, muumini Kingsley Adjei anaamini kwa dhati: "Hutibu roho kwa tembe. Unazivunja kwa maombi.”
Katika Kambi ya Pure Power Prayer Camp huko Adeiso, mhudumu Augustina Twumasi alisema vituo vya imani vinasaidia kuokoa mfumo dhaifu wa afya. "Kama si kambi za maombi, hospitali zingesambaratika kwa idadi ya wagonjwa,” alisema.
Lakini hali katika kambi nyingi ni duni. Wagonjwa hukaa kwenye sakafu za zege bila uingizaji hewa mzuri. Wengine wamekonda kwa utapiamlo, na baadhi wana alama za majeraha kutokana na kufungwa au kufungwa minyororo.
Licha ya marufuku ya mwaka 2017 dhidi ya kuwafunga wagonjwa wa akili, Human Rights Watch inasema vitendo hivyo bado vinaendelea kwa siri. Mwaka 2023, zaidi ya wagonjwa 30 waliokutwa wamefungwa waliokolewa katika Mkoa wa Mashariki pekee.
"Wanaendelea kuwafunga lakini huwaficha wageni au wanahabari wanapokuja,” kilisema chanzo cha usalama katika moja ya kambi hizo.
Imani, hofu na minyororo
Katika Hospitali ya Mafunzo ya Korle Bu, kituo kikuu cha rufaa nchini, daktari wa magonjwa ya akili Abigail Harding alisema imani inaathiri pakubwa namna Waghana wanavyoelewa afya ya akili.
Alionya kuwa kufungwa, kufunga kwa lazima na kutengwa kunaweza kuongeza majeraha ya kisaikolojia, kuchelewesha tiba sahihi na wakati mwingine kusababisha vifo.
Mwanasaikolojia wa kliniki wa Chuo Kikuu cha Ghana, Emmanuel Asampong, alisema suluhu si kuwatenga waganga wa imani kabisa, kwani wanaaminika na jamii. "Tunahitaji kuwashirikisha, kama ilivyofanyika kwa wakunga wa jadi,” alisema.
Kisheria, familia au polisi wanaweza kuomba matibabu ya lazima mahakamani iwapo mtu ni hatari kwa nafsi yake au kwa wengine. Lakini wengi hawajui sheria hiyo, alisema mwanasheria na mwanaharakati Lady-Ann Essuman.
MHA inasema imeanza kuwashirikisha viongozi wa dini kupitia mafunzo. "Dini ni sehemu ya utambulisho wetu,” alisema Josephine Stiles Darko. "Hatuwezi kuiondoa, lakini msaada wowote lazima uwe wa kibinadamu na ufuate sheria.”
Hata hivyo, hofu ya hospitali, matumaini ya miujiza ya haraka na unyanyapaa vinaendelea kuwavuta maelfu ya watu katika misitu na kambi. Utafiti wa Afrobarometer wa 2022 ulionyesha asilimia 60 ya Waghana wanaamini magonjwa ya akili husababishwa na uchawi au laana.
Jua lilipopanda juu ya Msitu wa Achimota, sauti za maombi ziliongezeka. Mwanamke aliyefikishwa kwa Nabii Ankrah hakusogea. Pembeni yake, dada yake alimshika mkono na kunong'ona kuwa uponyaji utakuja—ikiwa si leo, basi baada ya kufunga zaidi.