Wagonjwa wa Fistula bado wakabiliwa na unyanyapaa
23 Mei 2023Kwa karne nyingi maradhi hayo yamekuwa na athari kubwa za kijamii na kiuchumi hususani kwa wanawake.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘komesha fistulla' na huko nchini Uganda, jamii inasema ufadhili duni kwa mifumo ya afya ya uzazi unazidi kuchangia ongezeko la idadi ya waathirika.
Soma Pia: Adha wanazopata wagonjwa wa Fistula
Ugonjwa wa nasuri au kama ulivyozoeleka kwa lugha ya kiingereza kama Fistula bila shaka huwaweka waathirika na jamaa zao katika hali ngumu. Ugonjwa huu hutokea hasa pale mama mjamzito anapopata matatizo wakati wa kujifungua ambapo mifumo yake ya huhitilafishwa na kumsababisha kushindwa kudhibiti haja ndogo na kubwa kama ilivyo kwa watu walio katika hali sawa. Hii ina maana kuwa wakati wowote ule anaweza kuvuja na kuchafua nguo zake. Hiki ndicho chanzo cha unyanyapaa kwa mwaathirika na hata kwa watu wake wa karibu.
Soma pia: Uganda Kupambana na Ugonjwa wa Fistula
Takwimu za shirika la Afya
Kulinganana na takwimu za shirika la afya duniani, kila mwaka hadi wanawake laki moja katika mataifa yanayoendelea huugua nasuri kutokana na uzazi wenye hitilafu. Nchini Uganda pekee,idadi ya wanawake wanaougua ugonjwa huo ni hadi laki mbili. Juhudi za kutiba ugonjwa huo zimeimarika katika miaka ya hivi karibuni na idadi ya wanaopata tatizo hilo imepungua baada ya kushughulikiwa ipasavyo. Safari ya matibabu hata hivyo si rahisi kwa wengi kutokana na umbali wanakotoka kufika vituo vya afya na pia uwezo wao kimapato.
Baada ya kubaini kwamba ugonjwa huo wawezea kuepushwa, wadau na wataalamu wa afya wanalenga kuhakikisha kuwa hakuna tena nasuri duniani kufikia mwaka 2030. Lakini hilo litawezekana tu ikiwa ufadhili wa kutosha utatolewa kuwezesha kuwepo kwa mifumo thabiti ya afya ya uzazi. Wakunga wa kutosha waliopata mafunzo stahiki wanatakiwa kuwashughulikia ipasavyo akina mama wajawazito. Lakini zaidi ni kwamba jamii inamsaidia mama mjazito kufika kwenye kituo cha afya ili aweze kujifungua salama. Wakati huohuo, wasichana wanahimizhwa kujiepusha na mimba za utotoni kwami hawajakomaa kuweza kujifungua salama. Wanaweza kujikuta katika mashaka ya kuugua nasuri yaani fistula.