1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wagonjwa wa homa ya nyani wakosa dawa na chakula Kongo

3 Septemba 2024

Mamia ya wagonjwa wanalala kwenye magodoro membamba katika wodi ya muda iliyotengewa wagonjwa wa homa ya nyani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mgonjwa wa mpox akipakwa dawa DR Kongo
Mgonjwa wa mpox akipakwa dawa DR KongoPicha: WHO/Aton Chile/IMAGO

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ndio kitovu cha mripuko wa homa ya nyani ambayo Shirika la Afya Duniani WHO mwezi uliopita, liliitangaza kuwa dharura ya afya ya umma ulimwenguni.

Chanjo zinatarajiwa kufikishwa nchini humo katika muda wa siku chache zijazo kupambana na aina hiyo mpya ya virusi, wakati Rais wa nchi hiyo Felix Tshisekedi akiruhusu malipo ya kwanza ya dola milioni 10 ya chanjo hizo kukabiliana na mripuko huo.

Lakini katika hospitali moja mjini Kazimu, ambapo wagonjwa 900 wenye dalili za ugonjwa huo wamelazwa kwa muda wa miezi mitatu iliyopita, wafanyikazi wa afya wanahitaji msaada wa dharura.

Daktari mkuu hospitalini humo Musole Mulamba Muva, anasema wanaishiwa na dawa kila siku.

Soma pia: Uganda yatangaza kusambaa kwa homa ya nyani

Muva ameongeza kuwa kuna changamoto nyingi wanazojaribu kukabiliana nazo kwa njia zao katika eneo hilo na kusema misaada kutoka kwa mashirika ya kimataifa imepungua kwa kiwango kikubwa.

Wiki iliyopita, kulikuwa na wagonjwa 135 katika wodi hiyo ya mpox, watoto na watu wazima kwa pamoja wakirundikana katika hema tatu za plastiki zilizosimamishwa kwenye eneo lenye unyevunyevu ambalo halikufunikwa.

Jamaa ambao kwa kawaida hupeleka kiasi kikubwa cha chakula katika vituo vya umma vyenye ufadhili mdogo kama vile hospitali ya Kavumu, wamepigwa marufuku kutembelea wodi hiyo ya mpox ili kuepusha maambukizi.

Nzigire Lukangira, mama mwenye umri wa miaka 32 ambaye mwanawe mdogo amelazwa hospitalini humo, amesema hawana chochote cha kula.

Wagonjwa watumia dawa za kienyeji dhidi ya Mpox

Furaha Elisabeth anampaka dawa mtoto wake Sagesse Hakizimana aliyekutwa na ugonjwa wa Mpox katika kituo cha afya kilichoko Munigi, eneo la Nyiragongo, karibu na Goma jimbo la Kivu Kaskazini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Picha: Arlette Bashizi/REUTERS

Lukangira anasema wakati wanapoomba dawa za kushukisha viwango vya joto kwa watoto wao, hawapewi chochote.

Mkuu wa timu ya kukabiliana na mpox nchini Kongo, Cris Kacita, amekiri kwamba sehemu kadhaa za nchi hiyo zinakosa dawa na kwamba kutuma michango, ikiwa ni pamoja na tani 115 za dawa kutoka Benki ya Dunia ni suala la kipaombele.

Kama akina mama wengine katika wodi ya mpox katika hospitali ya Kavumba, Lukangira alikuwa ameanza kutumia dawa za kienyeji kupunguza maumivu ya mtoto wake.

Wanatumia maji ya limau yenye chumvi ama potassium bicarbonate kwenye malengelenge ya watoto wao.

Janga la homa ya nyani mkoa wa Kivu Kusini

04:02

This browser does not support the video element.

Wagonjwa watu wazima pia hujifanyia hivyo hivyo.

Visa vingi vya maambukizi vinatoka katika mji huo na vijiji jirani. Wodi nyingine mbili za muda zimejengwa katika eneo hilo.

Mwakilishi wa afya katika eneo hilo Daktari Serge Munyau Cikuru, ametoa wito kwa serikali kuendelea kushinikiza kupata chanjo hizo.

Kacita anasema watu wenye kiwango kikubwa cha hatari ya kuambukiza wengine, wamegunduliwa pamoja na maeneo tisa ya kipaombele kwa awamu ya kwanza ya chanjo.

Soma pia: WHO : Afrika inaweza kutokomeza Mpox ndani ya miezi sita

Kulingana na wizara ya afya nchini Kongo, kuliripotiwa visa 19,710 vya mpox kuanzia mwanzoni mwa mwaka hadi Agosti 31, na kati ya visa hivyo, 5,041 vilithibitishwa na wagonjwa 655 walikufa.

Mpox husababisha dalili kama za mafua na vidonda vilivyojaa usaha na wakati ambapo kwa kawaida ugonjwa huo hautishii maisha, unaweza kusababisha vifo.

Watoto, wanawake wajawazito na watu walio na kinga dhaifu wote wako katika hatari kubwa ya kukabiliwa na matatizo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW