1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahafidhina washinda uchaguzi nchini Ugiriki

8 Julai 2019

Kiongozi wa upinzani wa chama cha kihafidhina nchini Ugiriki  Kyriakos Mitsotakis ameshinda uchaguzi wa bunge uliofanyika jana Jumapili.

Parlamentswahl in Griechenland 2019 | Kyriakos Mitsotakis, Nea Dimokratia
Kiongozi wa Chama cha New Democracy Kyriakos Mitsotakis Picha: Reuters/E. Kafantari

Uchaguzi huo umetoa pigo kwa waziri mkuu Alexis Tsipras aliyeiongoza Ugiriki kwa miaka minne wakati wa mzozo mkubwa wa kifedha.

Chama cha New Democracy cha mwanasiasa Mitsotakis kimepata asilimia 39.8 ya kura ikilinganishwa na asilimia 31.5 za chama cha mrengo wa shoto cha Syriza cha waziri mkuu Tsipras.

Mitsotakis ameahidi kutimiza ahadi za kampeni ikiwemo kupunguza kiwango cha kodi, kuvutia uwekezaji na kubuni nafasi zaidi za kazi

"Wagiriki wanastahili kilicho bora. Na sasa ndiyo wakati wa kuthibitisha hilo kwa vitendo. Niliwaomba mnipe nguu ya kuibadilisha Ugiriki. Mmenipatia hilo kwa ukarimu tena mkipuuza  kebehi, migawanyiko na chuki na sitowaangusha." amesema Mitsotakis wakati wa hotuba yake ya kuzungumzia ushindi wa chama chake.

Mwanasiasa huyo ataapishwa baadae leo kuwa waziri mkuu wa Ugiriki na anatarajiwa kutangaza baraza lake la mawaziri muda mfupi baada ya kula kiapo.

Chama cha Syriza chaangukia pua

Waziri Mkuu wa Ugiriki, Alexis Tsipras anaondoka madarakani baada ya kushindwa uchaguzi.Picha: Reuters/A. Konstantinidis

Waziri Mkuu anayeondoka Alexis Tsipras alikubali kushindwa na alimpigia simu Mitsotakis kumpongeza kwa ushindi wa uchaguzi.

Kadhalika Tsipras amesema chama chake sasa kitafanya kazi ya kulinda maslahi ya wafanyakazi nchini Ugiriki kikiwa chama cha upinzani makini na kinachowajibika dhidi ya serikali.

"Ninataraji na kutumai kuwa kurejea kwa chama cha New Democracy madarakani hakutasababisha mparakanyiko hasa kwenye mafanikio yaliyokwishapatikana ya kulinda haki za walio wengi na za wafanyakazi. Syriza kitakuwa hapa kama chama imara cha upinzani na tutapambana kuzuia hilo" Tsipras aliwaambia wafuasi wake katika hotuba ya kukubali kushindwa.

Uchaguzi wa Ugiriki ulikuwa wa kwanza tangu nchi hiyo ilipoinukia tena kutoka mipango mitatu ya uokozi ambayo ilitegemea mafanikio ya hatua za kufunga mkaja ikiwemo kuongeza viwango vya kodi na kupunguza matumizi ya serikali.

Mgogoro wa kifedha ulishuhudia kiwango cha juu kabisa cha ukosefu wa ajira na umasikini pamoja na kuanguka kwa robo nzima ya uchumi wa Ugiriki.

Wapiga kura wa Ugiriki wakiadhibu chama cha siasa za mrengo mkali 

Wafuasi wa Chama cha Siasa kali cha Golden Dawn kilichopoteza uwakilishi katika Bunge nchini Ugiriki Picha: Getty Images/AFP/A. Messinis

Kwenye uchaguzi huo, chama cha mrengo mkali wa kulia cha Golden Dawn ambacho kiliundwa na wanazi mamboleo kimeshindwa kurejea bungeni katika matokeo yanayoashiria kuanguka uungwaji mkono wa chama hicho kilichokuwa cha tatu kwa ukubwa katika bunge la Ugiriki.

Chama hicho kimepata chini ya asilimia tatu ya kura, kiwango ambacho kimekinyima nafasi ya uwakilishi bungeni.

Matokeo ya uchaguzi huo yameonesha kuwa wapiga kura wa Ugiriki wamekataa mwenendo wa raia barani ulaya wa kuvichagua vyama vya siasa za mrengo mkali na zile zinazopinga Umoja wa Ulaya.

Waziri Mkuu Tsipras, aliitisha uchaguzi wa mapema baada ya chama chake kupata matokeo mabaya wakati wa uchaguzi wa bunge la ulaya na uchaguzi wa serikali za mitaa mwezi Mei na mapema mwezi Juni.

Mwandishi: Rashid Chilumba/

Mhariri: Iddi Ssessanga