Wahahriri: Urusi yataka kuonyesha bado ina nguvu
18 Juni 2015Gazeti la "Die Zeit" ambalo linatupa lawama kwa serikali ya Ugiriki. Mhariri wa gazeti hilo anasema: "Inawezekana kwamba serikali hii mpya imeundwa na watu wasio na ujuzi wa kisiasa. Lakini ukweli ni kwamba serikali hii haikuja hivi hivi. Ni matokeo ya serikali iliyokuwepo kabla kushindwa kutambua athari za kile walichokiita sera za uokozi. Vile vile ni matokeo ya viongozi wa Ulaya kukataa kuwanyang'anya matajiri wa Ugiriki fedha walizolimbikiza kimagendo bila kulipa kodi."
Gazeti la "Dithmarscher Lokalzeitung" linaangazia namna nchi zinazotumia sarafu ya Euro zinavyoshindwa kuwa na msimamo wa pamoja linapokuja suala la Ugiriki. Mhariri wa gazeti hilo anakumbusha kuwa Kansela wa Austria akiwa Athens aliihakikishia Ugiriki kwamba hakuna anayetaka kuona Ugiriki ikitolewa kwenye kundi la Euro. Lakini kura za maoni zinaonyesha kwamba wingi wa wananchi walioko kwenye ukanda wa Euro, hata Wajerumani, wanasema wamechoka na itakuwa sawa tu Ugiriki ikitolewa.
Putin atunisha misuli
Mada nyingine inayojadiliwa kwenye magazeti ya leo ni mvutano kati ya nchi za Jumuiya ya Kujihami NATO na Urusi. Baada ya Marekani kutangaza kwamba itaimarisha nguvu za kijeshi kwenye nchi mwanachama zinazopakana na Urusi, sasa Urusi nayo imesema itaongeza idadi ya makombora ya masafa marefu.
"Ujumbe wa Vladimir Putin kwa Marekani ni huu: mkiongeza kitisho dhidi yetu na sisi tutafanya hivyo hivyo," anasema mhariri wa gazeti la "Kölner Stadt-Anzeiger" na kuongeza: "Inashangaza kuona kwamba Urusi inatumia silaha za nyuklia katika vuta nikuvute hii ya kisiasa. Putin anataka kuukumbusha ulimwengu kwamba nchi yake bado ina nguvu, japokuwa si nguvu kubwa kama ilivyokuwa wakati wa kisovieti."
Lakini wapo pia wahahriri wanaomtetea Putin. Gazeti la "Augsburger Allgemeine" linakumbusha kwamba ununuzi wa makombora mapya ulikuwa sehemu ya mpango wa muda mrefu wa Urusi kuboresha shehena yake ya silaha za nyuklia. Mhariri huyo anaendelea kusema: "Hata Marekani inatekeleza mpango kama huo. Kwa hiyo uamuzi wa Urusi kununua makombora 40 haubadilishi chochote. Mpango huu ulikuwa wa muda mrefu, Putin ameamua kuutangaza sasa ili kuionyesha dunia kwamba nchi yake ina nguvu."
Mwandishi: Elizabeth Shoo
Mhariri: Josephat Charo