1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahamiaji 1,000 waokolewa pwani ya Italia

3 Machi 2017

Wahamiaji 970 waliokolewa katika ufukwe wa bahari ya Mediterenia katika pwani ya Libya siku ya Alhamis, wakati ambapo idadi ya wale wanaojaribu kuvuka bahari hiyo kuingia Ulaya inaongezeka.

Italien gerettete Bootsflüchtlinge im Hafen von Catania
Wahamiaji wakishuka kutoka kwenye boti ya walinzi wa pwani ya ItaliaPicha: Reuters/A. Parrinello

Kwa mujibu wa walinzi wa pwani ya Italia, hata kabla ya wahamiaji hao waliookolewa Alhamis, zaidi ya watu 13,400 walikuwa wamewasili katika fukwe za Italia mwaka huu, ongezeko la asilimia 50 hadi 70 ikilinganishwa na mwaka 2016 na 2015.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, UN, zaidi ya watu 440 walifariki au kupotea mwezi Januari na Februari wakati walipokuwa wakivuka kuingia Ulaya kutoka Libya, wakati wa msimu wa baridi, kipindi ambapo bahari huwa katika hali mbaya mno.

Wahamiaji hao waliookolewa walikuwemo kwenye boti nne za mpira, moja ndogo ya mbao na nyengine kubwa. Ulinzi wa pwani ya Italia unasema uliwasiliana na chombo kimoja cha Norway, meli mbili zinazotoa misaada ya kibinadamu, shirika la madaktari wasio na mipaka na shirika moja la misaada la Uhispania ili kufanya uokoaji huo.

Ulinzi huo wa pwani ya Italia unasema pia ulipokea ishara kutoka kwa boti moja iliyotokea Ugiriki ikiwa imewabeba wahamiaji 85 ikielekea kusini mwa Italia, lakini boti hiyo haikufanikiwa kuivuka bahari hiyo ya Ugiriki.

Ulaya yafunga njia ya wahamiaji kuingia barani humo

Boti hiyo iliokolewa na chombo kimoja kutoka Malta kilichokuwa eneo hilo wakati huo huo  wahamiaji waliokuwamo wakapelekwa katika bandari ya kusini mwa Ugiriki, iitwayo Kalamata.

Wahamiaji wa Afrika katika bahari ya MeditereniaPicha: picture-alliance/AP Photo/S. Diab

Juhudi za Ulaya kufunga njia ya wahamiaji iliyoko bahari ya Mediterenia huko Ugiriki, ndilo jambo linalodhaniwa kuchangia katika ongezeko la wahamiaji kuingia Italia, huku wengi wakianzia safari zao nchini Libya, kilomita 300 tu kutoka pwani ya Italia.

Mataifa ya Ulaya yanatafakari mbinu nyengine zinazolenga kuzuia kuwasili kwa wahamiaji katika nchi zao, jambo linaloyashtua makundi ya kutoa msaada yaliyo na wasiwasi kwamba huenda watu waliokwama nchini Libya wakapitia mateso.

Miaka sita baada ya kung'olewa mamlakani Moamar Gaddafi, Libya bado iko kwenye mzozo na taifa hilo limekuwa kama kituo cha wahamiaji kukutana wafunge safari ya kuingia Ulaya.

Wakimbizi na wahamiaji zaidi ya milioni moja wameingia ulaya tangu 2014

Wakati huo huo, afisa mkuu wa uhamiaji wa Umoja wa Ulaya EU huko Brussels, Ubelgiji, amesema mataifa wanachama wa Umoja huo, yanatakiwa kuwa tayari kuwazuia wahamiaji wasio na sababu ya kupata hifadhi, ili wasitoroke kabla hawajarejeshwa kwao.

Wahamiaji walia baada ya kuokolewa pwani ya ItaliaPicha: picture-alliance/AP Photo/S. Diab

EU inataka kupunguza uhamiaji baada ya wahamiaji na wakimbizi milioni 1.6 kufika katika fukwe zake kupitia Mediterenia mwaka wa 2014 hadi 2016. Umoja huo unataka kuwazuia watu kuingia kwenye nchi zao na iwarejeshe wengi zaidi makwao.

" Idadi ya wale wanaorudishwa kwao ni lazima iongezeka ,"alisema kamishna wa uhamiaji Dimitris Avramopoulos, "Nchi wanachama zinastahili kutumia uwezekano wa kuwaweka wahamiaji vizuizini kwa muda wa kutosha iwapo kuna hatari ya kutoroka, ili wakamilishe harakati za kuwarejesha katika nchi zao," aliongeza Avramopoulos.

Ubelgiji inakadiria kuna watu milioni moja katika mataifa ya Umoja wa Ulaya wanaostahili kurejeshwa makwao, lakini ni takriban theluthi moja ya hao tu ndio wanaorudishwa kwa sasa.

Mwanidishi: Jacob Safari/AFP/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman