1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahamiaji 300 hawajulikani waliko baharini Atlantiki

11 Julai 2023

Boti tatu zikiwa zimesheheni zaidi ya wahamiaji 300 zimetoweka katika Bahari ya Atlantiki kati ya bara la Afrika na visiwa vya Canary vya Uhispania. Wahamiaji 86 waliokolewa siku ya Jumatatu.

Baadhi ya wahamiaji kutoka Afrika katika bandari ya Tenerife visiwa vya Canary nchini Uhispania. (Picha ya maktaba ilipigwa 06.11.2007).
Baadhi ya wahamiaji kutoka Afrika katika bandari ya Tenerife visiwa vya Canary nchini Uhispania. (Picha ya maktaba ilipigwa 06.11.2007).Picha: Manuel Lerida/epa/dpa/picture alliance

 Taarifa kuhusu mkasa huo zimeeleza kuwa wahamiaji 86 waliokolewa siku ya Jumatatu.

Wahamiaji hao walikuwa kwenye boti tatu ambazo hazijulikani zilipo. Haijabainika ikiwa wahamiaji 86 waliookolewa ni miongoni mwa wale walioabiri boti hizo.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na Huduma ya Uokozi ya Uhispania kupitia ukurasa wake wa Twitter siku ya Jumatatu, maafisa waliokuwa kwenye ndege ya kutafuta manusura baharini, waliwaona watu waliokwama baharini umbali wa kilomita 140 kusini mwa kisiwa cha Canary. Wakaiarifu huduma yao, ambapo walituma boti yao ya uokozi kutoka eneo la Gran Canaria kwenda kuwaokoa watu hao.

Meli moja ya shehena ambayo imesajiliwa Panama ilikuwa karibu na boti ya wahamiaji, na iliwaokoa wahamiaji hao kabla ya boti iliyokuwa njiani kuwaokoa kuwasili.

Soma pia: Je, wasafirishaji haramu wa binadamu ni akina nani?

Machafuko yaliyoitikisa Senegal mwezi Juni yadaiwa kuchochea vijana wengi kuwa tayari kuikimbia nchi hiyo.Picha: Leo Correa/AP/picture alliance

Msemaji wa Huduma ya Uokozi Baharini Sea Rescue amesema "hakika hatujui idadi kamili ya boti ambazo hazijulikani zilipo. Lakini idadi ya watu walioziabiri, zinafanana na taarifa tulizo nazo”.

Machafuko ya siasa ya Senegal yazidisha idadi ya wahamiaji

Mnamo Juni 23, shirika la kutoa misaada la Uhispania Caminando Fronteras, liliripoti kwamba boti mbili zilizokuwa na watu 60 kila moja ziling'oa nanga kutoka Senegal kuelekea Canaries.

Siku nne baadaye, boti nyingine iliyowabeba wahamiaji 200 pia iling'oa nanga kutoka pwani hiyo ya Afrika Magharibi.

Soma pia: Shughuli ya kuwatafuta manusura wa ajali ya boti Ugiriki kumalizika

Shirika hilo limekuwa likiwasiliana na familia za wahamiaji waliofunga safari hizo, lakini wamewaambia kuwa hawajapokea mawasiliano yoyote kutoka kwao au kuwahusu.

Helena Maleno, afisa wa shirika la Caminando Fronteras ameliambia shirika la habari la Ujerumani DPA kwamba wana wasiwasi mwingi.

Meli zote katika eneo linalokisiwa boti hizo zilitoweka, ziliarifiwa siku kadhaa zilizopita ili kuwa macho na kuwa tayari kuwaokoa wahamiaji endapo wataonekana.

Hali ya wahamiaji Kusini mwa Jangwa la Sahara

01:30

This browser does not support the video element.

Polisi ya Uhispania pia iliziarifu mamlaka za Morocco.

Lakini msemaji wa Huduma ya Uokozi ya Uhispania hakueleza ikiwa walianzisha operesheni ya kuwatafuta wahamiaji hao.

Maleno aliikosoa Uhispania kwa kutumia tu ndege moja ya kuwatafuta manusura na ambayo ilitumika kwa saa chache tu angani kila siku.

Ameongeza kuwa "lau ingekuwa ni Wajerumani 300 ndio hawajulikani waliko baharini, kungekuwa na operesheni kubwa ya kuwatafuta”.

Atlantiki, Bahari yenye mawimbi makali na hatari

Wahamiaji wengi wanaotoka Afrika hutumia njia ya Bahari Mediterrania kueleka Ulaya kupitia nchi kama Libya na Italia. Lakini wengine huamua kutumia njia ya Bahari Atlantiki, kutoka magharibi mwa Afrika ambayo ni safari ya kilomita 1,700 hadi visiwa vya Canary.

Wahamiaji wengi kutoka Afrika hutumia njia ya bahari Mediterrania. Lakini wengine hutumia njia hatari ya bahari Atlantiki yenye mawimbi makali.Picha: Manuel Navarro/dpa/picture alliance

Inaripotiwa kuwa njia ya Bahari Atlantiki ni moja kati ya zile hatari zaidi kwa wahamiaji, kwa sababu mawimbi yake ni makali ikilinganishwa na ya Mediterrania.

Caminando Fronteras asema watu 778 pia wamekufa maji katika njia hiyo ya Bahari Atlantiki katika kipindi cha miezi sita tangu mwaka ulipoanza. Na kwamba huenda idadi ya vifo ambavyo hukosa kuripotiwa ikawa juu kuliko takwimu zilizopo.

Kulingana na shirika la Wahamiaji la Umoja wa Mataifa UNHCR, wahamiaji 7,278 kutoka Afrika wamefika visiwa vya Canary kati ya mwanzo wa mwaka huu hadi Julai 2.

Mnamo mwezi Juni, boti 19 zilizowabeba wahamiaji kutoka Senegal zilitia nanga katika visiwa vya Canary. Lakini hakuna hata mhamiaji mmoja kati yao ameshasajiliwa rasmi tangu mwanzo wa mwaka.

(Chanzo: DPAE)