1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahamiaji 40 wafariki baharini

15 Agosti 2015

Takriban wahamiaji 40 wamekufa Jumamosi (15.08.2015) katika sehemu ya kuhifadhi mizigo kwenye boti iliokuwa ikisafirisha kwa magendo kaskazini mwa Libya katika habari ya Mediterenia kutokana na kuvuta mafusho ya mafuta.

Manowari ya Italia katika harakati za uokozi Bahari ya Mediterenia.
Manowari ya Italia katika harakati za uokozi Bahari ya Mediterenia.Picha: picture alliance/ROPI/Italian Navy

Kamanda Massimo Tosi akizungumza kwenye manowari ya Italia ya Cigala Fulgosi wakati opereseheni ya uokozi ikiendelea amesema kwamba wahamiaji waliokufa wamepatikana wakiwa kwenye eneo la kuhifadhi mizigo ndani ya boti hiyo na kwamba wengine 320 wameokolewa na manowari ya Italia.

Amesema wakati waokozi walipoingia kwenye boti hiyo miili ya wahamiaji ilikuwa imelala ndani ya maji,mafuta na kinyesi cha binaadamu kwenye eneo la kuhifadhia mizigo

.Kwa mujibu wa Waziri wa mambo ya ndani wa Italia Angelino Alfano idadi ya vifo inaweza kuongezeka kutokana na kuendelea kuhesabiwa kwa wahanga.

Manusura ni pamoja na watoto watatu na wanawake 45 ambao walikuwa wakiwalilia waume zao na watoto wao waliokufa wakati wa msafara huo.Katika sehemu nyengine ya bahari hiyo ya Mediterenia wahamiaji katika pwani ya Uturuki walikuwa wakigombania nafasi kwenye mojawapo ya boti za mipira wakitapatapa kuizuwiya isizame wakati wa usiku jambo ambalo limeonyesha kutapatapa kwao kufikia kisiwa cha Ugiriki cha Kos na usalama wa Ulaya.

Wahamiaji watapia kuingia Ulaya

Mandhari hiyo iliochukuliwa na waandishi wa habari wa shirika la habari la AP kwenye usiku usiokuwa na mbaa la mwezi inakuja wakati serikali ya Uturuki ikirepoti kwamba wahamiaji 2,791 wamegundulika katika Bahari ya Aegean katika kipindi cha siku tano zilizopita wengi wao wakitokea Syria.

Mhamiaji akiokolewa na helikopta Bahari ya Mediterenia.Picha: Italian Navy

Kos iko kama kilomita nne tu kutoka Uturuki ambacho ndio kituo cha karibu kabisa na taa zake zinazometa wakati wa usiku ni kivutio kwa wakimbizi hao wanaokimbia vita na umaskini.

Adimeri wa manowari ya Italia mwenye kuratibu shughuli za uokozi baharini amesema kundi la kwanza la wahamiaji waliokolewwa katika boti mbili za mpira walisogelea manowari yao kwa uangalifu kwani mara nyingi wahamiaji huelemea upande mmoja wa vyombo vyao wakati wapongunduwa msaada jambo linapelekea kupinduka na kuzama kwa mashua zao.

Adimeri Pieerpaolo Ribuffo amekaririwa akisema "Tumeshuhudia boti hiyo ikiwa imefurika wahamijai katika kiwango kisichowazika."

Maelfu wahatarisha maisha

Maelfu ya wahamiaji wamekuwa wakiendelea kuhatarisha maisha yao kupitia bahari ya Mediterenia mwaka huu wakitaraji kufika Ulaya na kupewa hifadhi.Wanakimbia vita,ukandamizaji na umaskini Mashariki ya Kati,Afrika na Asia.

Wahamiaji wakiwasili katika kisiwa cha Kos nchini Ugiriki.Picha: Getty Images/AFP/L. Gouliamaki

Wahamiaji wanaokadiriwa kufikia 2,300 wamekufa baharini mwaka huu wakijaribu kuvuka bahari.Njia kati ya Libya na Italia inatajwa kuwa ndio mbaya kabisa idadi hasa ya watu waliopoteza maisha yao kamwe haiwezi kujulikana kutokana na kwamba baadhi ya mashua hizo za kusafirisha watu kwa magendo inaaminika kwamba zimezama baharini bila ya waokowaji kutambuwa.

Idadi ya wahamiaji wanaojaribu kuingia Ulaya kwa njia ya bahari inatazamiwa kuvunja rekodi mwaka huu.Ugiriki imeripoti kuwasili nchini humo kwa wahamiaji 134,988 mwaka huu kwa kupitia Uturuki.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP

Mhariri : Yusra Buwayhid

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW