JangaLibya
Wahamiaji 61 wapoteza maisha baharini njiani kwenda Ulaya
17 Desemba 2023Matangazo
Taarifa hizo zimetolewa na Shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa IOM kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X.
Ikiwanukuu manusura wa mkasa huo, IOM imesema boti hiyo iliyokuwa imewabeba watu wasiopungua 86 iling´oa nanga kwenye mji wa mwambao wa Zuwara ulio umbali wa kiasi kilometa 110 kutoka mji mkuu wa Libya, Tripoli.
Inaarifiwa kuwa mawimbi makubwa yaliipiga boti hiyo na kuwa chanzo cha ajali iliyogharimu maisha ya watu 61.
Ajali hiyo ya jana Jumamosi ndiyo mkasa wa hivi karibuni kabisa kwenye mfululizo wa masaibu yanayowakumba wahamiaji wanaotumia njia hatari kujaribu kuingia barani Ulaya.
Umoja wa Mataifa unakadiria watu 2,200 wamekufa ndani ya mwaka huu pekee kwa kuzama baharini wakiwa njiani kukimbilia nchi za Ulaya.