Merkel: wahamiaji changamoto kuliko deni la Ugiriki
17 Agosti 2015Akizungumza na kituo cha televisheni cha ZDF mjini Berlin kupitia kipindi maalum cha mahojiano ya majira ya kiangazi hapo jana usiku, Kansela Merkel alisema mmiminiko wa wakimbizi barani Ulaya utalikabili bara hili kwa kipindi kirefu zaidi kuliko inavyodhaniwa na linapaswa kupewa umuhimu mkubwa kwenye mipango ya sasa na ya baadaye ya viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya.
"Ninaamini kuwa kama ambavyo tunazungumza juu ya Ugiriki, tunapaswa pia kujiuliza ni vipi tunashughulika na suala la wakimbizi, vipi tunashughulika na majirani zetu nchi za Kiafrika, tutapaswa kujiuliza ikiwa kunawezekana kupatikana suluhisho la kidiplomasia kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe. Masuala haya yatatuandama kwa muda mrefu zaidi kuliko suala la madeni ya Ugiriki na uthabiti wa sarafu ya euro," alisema Merkel.
Licha ya Ujerumani kutajwa kuwa moja ya nchi za Ulaya zinazopokea wakimbizi kwa wingi katika siku za karibuni, Kansela Merkel alisema bado nchi yake haijaelemewa sana na mzigo huo na badala yake akatowa wito kwa Wajerumani kuendelea kukunjua mikono yao kuwapokea wale wenye shida, na akilaani vikali tabia za hivi karibuni za wenyeji kushambulia makaazi ya muda yanayowahifadhi wakimbizi.
"Hilo ni jambo lisilotustahikia nchini mwetu. Hakuna uhalali wa kufanya hivyo. Ghasia dhidi ya vituo vya waomba hifadhi, ghasia dhidi ya wakimbizi. Kila mtu anayekuja hapa ni mwanaadamu na ana haki ya kutendewa kama mwanaadamu."
Hata hivyo, Merkel alionya kwamba changamoto hiyo haiwezi kukabiliwa kwa kufanya kazi kwa mazoea. Amekiambia kituo cha ZDF kwamba tayari ameshazungumza na Rais wa Kamisheni ya Ulaya, Jean-Claude Juncker, juu ya haja ya Umoja wa Ulaya kuanzisha sera ya pamoja ya waomba hifadhi. Merkel anatazamiwa pia kulizungumzia suala hilo na Rais Francoise Hollande wa Ufaransa.
Ugiriki haitapunguziwa madeni
Wizara ya Ndani ya Ujerumani inakisia kuwa kufikia mwishoni mwa mwaka huu, wahamiaji 450,000 watakuwa wameomba hifadhi, ingawa nusu ya waliokwishawasili hadi sasa ni kutoka nchi za Balkan, ambao hawana sifa ya kupatiwa hifadhi.
Wakati huo huo, Kansela Merkel ametetea msimamo wa nchi yake kuelekea mzozo wa madeni wa Ugiriki, akisema anakubaliana na uwezekano wa kuipa muda zaidi nchi hiyo kulipa madeni yake, lakini haafiki suala la kupunguziwa madeni hayo.
"Kuhusiana na uongezaji wa muda wa malipo, upangaji wa viwango vya riba, inawezekana tuna namna ya kufanya kama ambavyo tulifanya huko nyuma. Tuliongeza muda wa malipo, tulisogeza mbele viwango vya ulipaji, lakini kuna kauli ya wazi kwamba Kanda ya Euro haiwezi kuruhusu upunguzaji madeni," alisema Merkel.
Kiongozi huyo wa Ujerumani amesisitiza kuwa yuko tayari kuzungumzia ahuweni hiyo ya deni kwa kuzingatia pia misingi ya kibinaadamu, na kuifanya Ugiriki isijione imetengwa ndani ya Kanda ya Euro.
Wabunge kadhaa wa muungano wa CDU/CSU wamejitokeza kuzuia mipango ya kupinga awamu nyengine ya fedha za uokozi kwa Ugiriki katika kikao maalum kinachofanyika keshokutwa, Jumatano.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/dpa
Mhariri: Josephat Charo