Wahamiaji kurejeshwa makwao na polisi kupatiwa kinga
9 Februari 2017Kansela Angela Merkel anapanga kutangaza mpango wa vifungu 16 wenye lengo la kuharakisha kurejeshwa makwao wale wote ambao maombi yao ya ukimbizi hayana nafasi ya kukubaliwa. Kuhusu mpango huo linaandika gazeti la "Lausitzer Rundschau": "Yadhihirika kana kwamba kansela alibidi kwanza kujifunza kwamba kati ya maneno na vitendo kuna tofauti kubwa. Ni rahisi kusema, asiyeruhusiwa kusalia anabidi aende zake, utekelezaji wa maneno hayo lakini ni mgumu kutokana na mfumo wa shirikisho. Na hapo hatukuitaja mitihani mingine ya kibinaadamu. Katika suala hili Merkel anajikuta akikabwa na shinikizo la kisiasa. Kutoka kwa wananchi wasiotaka kuelewa na pia kutoka chama cha siasa kali za mrengo wa kulia Chaguo Mbadala kwa Ujerumani AfD, bila ya kuwataja wakosoaji wake ndani ya vyama ndugu vya kihafidhina na hatimae bila ya shaka ile hali ya kuzidi kupata nguvu chama cha Social Democrat baada ya Martin Schulz kuteuliwa kugombea kiti cha kansela.
Hatua za serikali kupambana na matumizi ya nguvu dhidi ya polisi
Mada yetu ya pili magazetini inahusu hatua za kupatiwa kinga polisi dhidi ya hujuma katika jamii. Serikali kuu ya Ujerumani imepitisha sheria kukabiliana na hali hiyo. Gazeti la "Rheinpfalz" linaandika: "Hatua ya serikali si chochote chengine isipokuwa ishara tu kwa polisi kwamba kilio chao kinazingatiwa. Mtu anaweza kusema, serikali inataka kuonyesha inawajibika. Na hatua hiyo haigharimu chochote. Hicho ni kiini macho kwasababu anaezingatia kwa dhati kilio cha polisi anabidi apanie kweli kweli.
Nalo gazeti la "Badische Zeitung" linasema: "Matarajio kwamba kuzidisha makali sheria kutasaidia kuwapatia kinga polisi, hayatekelezeki. Kwasababu mtu aliyepandisha au aliyelewa, mara nyingi hafikirii madhara ya kitendo chake. Kwa hivyo yadhihirika kana kwamba wanasiasa wametaka kuwaonyesha polisi kwamba hatua zinachukuliwa, lakini bila ya kugharimu chochote. La maana zaidi lingekuwa kama mishahara ingeongezwa na vifaa kuzidishwa-lakini hilo lingegharimu pesa ndio maana imepitishwa sheria ambayo mtu anaweza kusema "ni ya daraja ya pili."
Malipo ya uzeeni yadhaminiwe
Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu hali ya umaskini miongoni mwa wazee. Gazeti la "Mannheimer Morgen" linaandika: "Fikra ya kulazimishwa kisheria kutengwa kiwango maalum cha malipo ya uzeeni inatia moyo. Inadhamini hakuna anaestahiki kulipwa na kuishi chini ya kiwango hicho. Na hali hiyo itapelekea kufanyiwa marekebisho mfumo mzima hadi kuhakikisha malipo ya uzeeni yanatokana na fedha za walipa kodi. Jambo hilo linawezekana kwasababu nchi za Skandinavia zinafuata tayari utaratibu huo.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir
Mhariri:Yusuf Saumu