1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahamiaji wa Wafanyakazi wa Kimataifa

Charles Hilary7 Juni 2006

Hisia zilizozoeleka juu ya suala la uhamiaji wa kimataifa,polepole sasa zinaanza kufifia,baada ya kugundulika ongezeko kubwa la wafanyakazi wahamiaji na wale wenye utaalam,wakihama kutoka nchi moja inayoendelea kwenda nyingine ambayo nayo imo katika mchepuo wa kujikwamua kiuchumi Hayo yamo katika ripoti ilitolewa na Umoja wa Mataifa jana.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,Kofi Annan.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,Kofi Annan.Picha: AP

Katika ripoti yenye kurasa 90 iliyopewa jina Uhamiaji wa Kimataifa na Maendeleo, iliyosomwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,Kofi Annan,imeelezwa kwa sasa hakuna shaka yoyote kuwa idadi kubwa ya wahamiaji wamekusanyika katika mataifa machache yanayoendelea yenye viwanda na hapa ikimaanishwa mataifa ya Magharibi.

Imeelezwa ndani ya ripoti hiyo kiasi cha wahamiaji wanaofikia milioni 200,wameondoka katika nchi zinazoendelea pia kwenda katika nchi nyingine za viwanda,huku ripoti hiyo ikizidi kubainisha idadi inayolingana na hiyo,wametoka mataifa masikini na kuhamia nchi zinazoendelea.

Kwa maneno mengine anasema Bwana Annan,wale wanaotoka nchi za kusini kwenda nyingine za kusini,wanalingana kwa idadi na wale wanaotoka kusini kwenda mataifa ya kaskazini,ambayo kwa asili yamekuwa yakifurika wahamiaji.

Balozi Prasad Kariyawasam kutoka Sri Lanka ambaye aliongoza kikao cha Umoja wa Mataifa kilichozungumzia wahamiaji wafanyakazi,ameeleza kuwa uhamiaji wa kimataifa kwa sasa sio suala la wale kutoka nchi changa kiuchumi kwenda mataifa yaliyoendela bali sasa limekuwa ni suala la kidunia zaidi.Ameongeza kueleza balozi Kariyawasam kuwa ongezeko la idadi ya wahamiaji wafanyakazi, wengi hivi sasa wameajiriwa katika mataifa yanayoendelea,ambayo yanalipa kiwango kikubwa cha mishahara hasa nchi za Mashariki ya Kati.

Kwa mujibu wa utafiri ulioondeshwa na Umoja wa Mataifa,mwaka jana wa 2005 idadi ya wahamiaji wa kimataifa ilifikia milioni 191,milioni 115 wakiwa wanaishi mataifa yaliyoendelea na waliobakia milioni 75 wanafanyakazi katika nchi zinazoendelea.

Kiasi cha karibu wafanyakazi wahamiaji wa kimataifa sita kati ya kumi wanaishi katika mataifa yenye uchumi uliotononoka,lakini pia zikijumuisha nchi zinazoendelea kama Bahrain,Brunei,Kuwait,Qatar,Korea ya Kusini,Saudi Arabia na Falme za Kiarabu.

Katika ripoti hiyo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofii Annan,amependekeza kuwepo na mkutano wa jukwaa la mataifa ya dunia 191,ambao utakuwa na jukumu la kuunda sera zenye mawazo mapya na kutia shime muelekeo wa kuwakubali wafanyakazi wahamiaji wa kimataifa kwa ajili ya maendeleo ya kitaifa na kimataifa.

Robo tatu ya wafanyakazi wahamiaji wote kwa mwaka jana wa 2005 waliishi katika nchi zisizozidi 28,huku kila mfanyakazi mmoja kati ya watano wahamiaji duniani,akiwa anaishi nchini Marekani.

Wakati huo huo,kumekuwa na mtandao wa mageuzi mapya kuhusiana na wahamiaji wa kimataifa,ili waweze kurejea makwao.Mathalan China na Korea ya Kusini,wamekuwa wakitoa vivutio kwa wataalam wao wa masuala ya utafiti wa kisayansi,wakubali kurejea nyumbani.

Wakati huo huo,mapendekezo ya kuwepo mkutano wa kimataifa kuhusu wahamiaji umekuwa ukipigwa danadana,katika mfumo wa Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha muongo moja sasa,lakini bila ya kutolewa maamuzi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW