Wahamiaji waendelea kumiminika Ujerumani
7 Septemba 2015Ujerumani ambayo imefungua milango yake kwa ajili ya kuwapokea wahamiaji wengi, imesema vyama vinavyounda serikali ya muungano vimefanya uamuzi wa kutenga fedha za umma kiasi cha euro bilioni 6, kufidia gharama za kuwashughulikia wahamiaji hao. Fedha hizo zitapatikana kuanzia mwaka ujao.
Chama cha kihafidhina cha CDU pamoja na chama cha SPD vimesema hayo katika taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya majadiliano ya jana usiku na kuongeza kuwa serikali ya muungano ya Ujerumani itaongeza bajeti yake ya mwakani kwa kiasi cha euro bilioni 3 ili kukabiliana na hali hiyo ya wakimbizi wanaotafuta hifadhi, halikadhalika serikali za majimbo pamoja na seriklai za mitaa nazo kwa upande wao zitatoa euro bilioni 3.
Na kulingana na afisa wa kituo cha reli mjini Munich katika jimbo la Bavaria, wahamiaji 10,000 wanatarajiwa kuwasili leo wakiwa wanatokea nchini Hungary na Austria. Ujerumani inatarajiwa kupokea wahamiaji 800,000 ndani ya mwaka huu.
Hungary, Uingereza na Ufaransa
Kwa upande wa Hungary, Waziri Mkuu wa nchi hiyo Viktor Orban akizungumza na wanadiplomasia katika mji mkuu Budapest leo amesema kuwa Umoja wa Ulaya unalazimika kuzipatia msaada Uturuki pamoja na nchi nyengine zisizokuwa wanachama wa muungano huo, ili kuzisaidia kukabiliana na wimbi hili la wahamaiji wanaotafuta hifadhi barani Ulaya.
Kiongozi huyo wa chama cha mrengo wa kulia ameongeza kuwa mjadala wa kugawana jukumu la kupokea wahamiaji baina ya nchi wanachama 28 wa Umoja wa Ulaya, hauna mana ikiwa nchi hizo zinashindwa kulinda mipaka yake.
Na Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron anatarajiwa kutangaza mipango yake ya kupokea wahamiaji 10,000 kutoka Syria baada ya kubadilisha msimamo wake wiki iliyopita kufuatia kusambaa kwa picha katika mitandao ya kijamii zinazoonesha hatima ya kusikitisha ya wahamiaji wanaojaribu kukimbilia Ulaya. Naye Rais wa Ufaransa Francois Hollande amesema kuwa Ufaransa itapokea wahamiaji 24,000 katika kipindi cha miaka miwili ijayo.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/dpae/afpe/rtre/ape
Mhariri:Yusuf Saumu